Unayafahamu mambo ya kuzingatia unapotaka kupakua App Playstore? Teknokona leo tumekuandalia orodha ya mambo muhimu ya kuzingatia unapotaka kupakua App Playstore. Kwa wasiofahamu Playstore ni soko la kupakua App mbalimbali mtandaoni kwaajili ya kutumia kwenye simu janja yako.
Kwa kutumia Playstore unaweza kupakua magemu ya simu, App za mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter na WhatsApp. Pia kwa simu janja zinazotumia programu endeshi ya Android huwa zinakuja na baadhi ya App kama Playstore yenyewe, Google pamoja na App zingine za kuanzia.
Miongoni mwa mambo ya kuzingatia unapotaka kupakua App Playstore ni pamoja na:
Kusoma maoni ya watu wengine kuhusu App hiyo unayotaka kupakua: Hii itakusaidia kupata uhalisia wa matarajio yako na hiyo App. Kwa kusoma maoni ya watu wengine utaweza kufahamu kero mbalimbali za watumiaji wa hiyo App unayotaka kupakua na kuweza kutafakari kwa kina kama bado unataka kupakua App hiyo.
Kuangalia Ukadiriaji (Ratings) wa App hiyo unayotaka kupakua: Playstore inaruhusu kila mtumiaji wa App flani kuikadiria ubora wake na kuonyesha wastani wa makadirio hayo wazi kabisa kwenye kurasa ya App hiyo ili watumiaji wapya waweze kuona makadirio ya kuridhishwa na huduma yanayotolewa na watumiaji wa App hiyo.
Kusoma taarifa za App unayotaka kupakua: Ni muhimu kusoma taarifa za juu juu kuhusu hiyo App ili kuepuka kukwazika na huduma utakazozikosa katika App hiyo kwa kigezo cha kuhisi kuwa App hiyo inaweza kuwa na huduma hizo.
Kusoma sera ya Faragha ya App unayotaka kupakua: Utakaposoma sera ya faragha ya App utaweza kufahamu ni taarifa zako zipi ambazo zitakusanywa na waendeshaji wa hiyo App na zitatumika vipi. Hili ni swala la muhimu kuzingatia kwasababu utakapokubaliana na sera hii utakuwa umewaruhusu wao kufanya mambo yote waliyoyaelezea kwenye sera yao bila ya wewe kuwashtaki iwapo hautapendezwa na matumizi yao ya taarifa zako.
Kuangalia ni aina gani ya ruhusa utatakiwa kutoa kwenye simujanja yako ili uweze kuitumia kwa ufanisi App hiyo. Mara nyingi hii huambatana na mambo yaliyozungumziwa kwenye sera ya faragha ya App, Ambapo maelezo ya kina yatatolewa kuhusiana na kila ruhusa ya ziada itakayohitajika kutoka kwa mtumiaji. Mfano wanaweza wakasema kuwa wanahitaji uruhusu uwezo wa App kutambua ulipo kwa wakati halisi ili waweze kukutumia taarifa sahihi kulingana na eneo ulilopo.
No Comment! Be the first one.