Watengenezaji mashuhuri wa simu zinazotumia Android, Samsung, waendelea kupata mapato madogo kabisa katika biashara zao kutokana na mauzo madogo ya simu zake janja kuliko ilivyotarajiwa. Katika miaka ya hivi karibuni kampuni hiyo imekuwa ikizidi kushuhudia mapato yake yakishuka sana.
Kampuni ya Samsung inavitengo vingi vya biashara lakini kitengo cha biashara ya uuzaji simu janja ndicho kilichokuwa kinaingiza mapato mengi zaidi na hivyo kuwatengenezea faida nono zaidi, lakini hili si linalotokea kwa sasa.
Katika kipindi cha mwezi wa nne hadi wa sita mapato ya kampuni hiyo yalishuka kwa takribani asilimia 8, na katika kushuka huko kwa mapato kitengo cha biashara za mauzo ya simu na tebleti mauzo yalishuka kwa asilimia 38%. Yaani kwa ufupi kitengo cha biashara za simu ndicho kinachoongoza zaidi katika ushukaji wa mauzo.
Wengi walitarajia ujio wa simu za Galaxy S6 na S6 Edge kuweza kukuza mapato ya kampuni hiyo, lakini hicho si kilichotokea. Galaxy S6 Edge ndiyo iliyouzika zaidi kiasi cha Samsung kujikuta katika hali ya kutojiandaa kabisa, kwani walikuwa wametengeneza Galaxy S6 nyingi zaidi kuliko S6 Edge. Hali hii inasemekana imechangia kwa kiasi kikubwa kwao kutofanya vizuri kimauzo kufikia malengo yao.
Tokea Apple na makampuni mengine kama vile Huawei waje na uamuzi wa kutengeneza simu zenye umbo kubwa kufikia zile za Samsung katika mwaka 2013 wamefanikiwa kuchukua soko kwa kiasi kikubwa kutoka kwa Samsung katika baadhi ya nchi za Asia kama vile Uchina ambapo watu wa huko wanapenda simu zenye maumbo makubwa. Ila ushukaji huu wa mapato ni mdogo ukilinganishwa na kipindi cha miezi minne kabla yake.
Soko la Uchina limekuwa moja ya soko muhimu sana la simu kwa kampuni inayotaka kufanikiwa kimauzo, na nchini humo tayari Samsung wanapata ushindani mkubwa kutoka kwa iPhones na Xiaomi. Kampuni ya Xiaomi ni moja ya kampuni inayokuja juu kwa kasi sana kimauzo nchini humo na duniani kote.
No Comment! Be the first one.