Marekani wazidi kuibana Huawei, tangu vyombo vya usalama na kisheria kuanza kuishutumu na ata kuifungulia mashtaka kampuni hiyo mambo hayajawa mazuri kwa Huawei.
Ndani ya muda mfupi tayari Huawei wamejikuta wakikosa biashara ambazo nyingine zilikuwa tayari kwenye hatua nzuri sana kwenye mataifa kadhaa.
Hadi sasa serikali ya Marekani imeifungulia mashtaka 2 kampuni ya Huawei nchini Marekani.
- Shitaka la kwanza ni kwa kutengeneza kampuni nyingine na hivyo kuendeleza biashara na taifa la Irani kitu ambacho ni uvunjifu wa sheria zinazotokana na vikwazo vya Marekani vya kibiashara kwa Irani. Kupitia shitaka hili tayari Mkurugenzi mkuu wa masuala ya fedha -Huawei, Bi. Meng Wanzhou anashikiliwa nchini Kanada, alipoenda kikazi, akisubiri kusafirishwa chini ya ulinzi hadi Marekani. (Bi Meng ni mtoto wa mwanzilishi wa kampuni hiyo)
- Shitaka la pili linahusisha wizi wa teknolojia kutoka kwa kampuni ya kimarekani ya T-Mobile. Wizi huo unasemakana ulifanyika mwaka 2012 ambapo wanadaiwa waliiba teknolojia ya utengenezaji wa roboti anayehusika na kuangalia ubora wa simu.
Katika yote haya kitu kikubwa kinachoonekana ni vita kubwa ni juu ya teknolojia ya 5G. Teknolojia ya 5G inaonekana kuwa ni moja teknolojia muhimu zaidi kwa sasa na kwa miaka mingi ijayo.
Teknolojia ya 5G Inategemewa kutumika katika vifaa vingi zaidi; vikihusisha vifaa vyote vya teknolojia vitakavyokuwa vinatumia intaneti ambavyo vinazidi kuongezeka; mfano magari, mafriji, mifumo ya taa za majumbani, n.k (vifaa vinavyotegemea Artificial Intelligence). Hadi sasa bado kampuni ya Huawei ndio kinara katika mikataba ya miradi ya kufunga mfumo wa 5G katika mataifa mengi duniani.
Huawei tayari wamejiweka katika nafasi ya juu sana katika teknolojia ya utengenezaji wa mifumo mikubwa ya mawasiliano kwa ajili ya mitandao ya simu na vyombo vya mawasiliano ya nchi. Wasiwasi mkubwa kwa Marekani ni kwamba ukaribu mkubwa wa kampuni ya Huawei kwa serikali ya Uchina unaweza ukawa umeshasababisha teknolojia za udukuzi wa data za mawasiliano kuweza kutumwa kwenda kwa vyombo vya kijasusi vya nchi hiyo (Uchina).
Je, madai haya yana ukweli wowote?
Hadi sasa bado hakuna taifa lililokuja na uthibitisho wa jambo hilo. Ila kupitia ushawishi wa Marekani tayari kampuni hiyo imeshapigwa chini katika kufunga mitandao ya 5G nchini Kanada, Australia.