Huduma ya Intaneti yenye kasi zaidi ya teknolojia ya 5G imeanza kutolewa na mashirika ya mawasiliano ya simu nchini China katika zaidi ya miji 50.
Huduma hiyo ilitangazwa kuanza na Mashirika matatu ya umma ya mawasiliano ya China. Mashirika hayo ni China Telecom, China Mobile na China Unicom.
Mashirika hayo yalitoa taarifa kwamba kuanzia Ijuma iliyopita katika miji ya Beijing, Shanghay,Hangzou, Guangzou na miji mingine mikubwa huduma ya 5G itaanza kupatikana.
Takribani vituo 50,000 vya 5G vimewekwa katika miji 50 ya nchini China
Teknolojia ya 5G inasifika kwa kuwa na kasi kubwa zaidi, huwezesha muunganiko wa simu za video kwa kasi kubwa na michezo ya simu huweza kutumika kwa ufanisi zaidi.
Mataifa mengine ambayo tayari yameanza kuwa na mitandao ya huduma za 5G, ingawa bado si kwa kiasi kikubwa kama cha China, ni pamoja na Korea Kusini, Marekani, na Uingereza.
Teknolojia ya 5G imechukuliwa kama moja ya teknolojia muhimu zaidi kwa ajili ya kujenga uchumi wa kisasa. Biashara na viwanda vitakavyoweza kutumia teknolojia hii vinategemewa kuwa na ufanisi wa hali ya juu zaidi ukilinganisha na watakaokuwa wanatumia teknolojia za nyuma.