Matangazo ya kisiasa kwenye Twitter na app/mitandao mingine ya kijamii kama Facebook yamekuja kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni. Suala la jinsi mitandao ya kijamii ilitumika katika matangazo ya kisiasa nchini Marekani kwenye uchaguzi uliopita limeleta mijadala hadi leo hii.
Katika uamuzi uliotangazwa na mkurugenzi na mwanzilishi wa Twitter Bwana Jack Patrick Dorsey, amesema kampuni hiyo imeamuza kuzuia kabisa matangazo yote yanayohusisha siasa – matangazo pekee yanayohusisha siasa yatakayoruhusiwa ni yale yanayohusu kuhamasisha watu wote kujiandikisha na kushiriki kwenye uchaguzi.

Uamuzi huu umekuja siku chache baada ya mkurugenzi wa Facebook, Bwana Mark Zuckerberg kuwekwa kitimoto na tume ya bunge la Marekani akitakiwa kujibu atachukua hatua gani kuzuia baadhi ya matangazo ya kisiasi yenye lugha ambazo zinaweza chukuliwa kama za chuki au habari za uongo. Katika kikao hicho Bwana Zuckerberg alisema hawataweza kuzuia matangazo ya wanasiasa kwa namna yeyote kwa kuwa kufanya hivyo itakuwa kuingilia misingi ya uhuru wa maoni ambao upo kwenye katiba ya Marekani.

Uamuzi huu wa Bwana Jack unaonekana kwenye kinyume kabisa na utetezi uliotolewa na Bwana Zuckerberg.
Kiuhalisia Twitter inatumika kwa kiasi kidogo tuu kwenye soko zima la matangazo ya kimtandaoni na uamuzi huu unaonekana wa kuonesha mfano lakini si kwamba utawaathiri sana wanasiasa ukilinganisha kama uamuzi huo ungechukuliwa na Facebook.
Katika uchaguzi wa 2016 watafiti wanaamini utumiaji mzuri wa Facebook ulichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kampeni ya Trump dhidi ya Clinton. Kampeni ya Trump ilitumia dola milioni 44 kwenye matangazo ya Facebook ukilinganisha na dola milioni 28 za Hillary Clinton.
Ili kuhakikisha ufanisi mkubwa wa matangazo, kampeni ya Trump ilitengeneza matangazo bora na mengi zaidi na kuhakikisha yanawafikia watu sahihi zaidi ukilinganisha na matangazo ya kampeni ya Clinton.
- Ingawa Facebook inawatumiaji zaidi ya milioni 200 wa Facebook, kwa wastani kampeni ya Trump ilitengeneza tangazo moja kwa lengo la kufikia watu husika milioni 2.5 tuu, wakati kampeni ya Clinton ilitengeneza tangazo moja kwa ajili ya watu milioni 8.
- Kwa ujumla wake kampeni ya Trump ilikuwa na matangazo zaidi ya milioni 5.9 ya kitofauti kwa ajili ya kuwafikia watu tofauti, kampeni ya Clintoni ilikuwa na matangazo takribani 66,000.
Hii inakupa picha jinsi gani kampeni ya Trump ilitumia vizuri teknolojia za kimatangazo ya mtandao kuhakikisha unatengeneza matangazo spesheli kwa ajili ya watu wa aina flani tuu. Na ni suala hili ndio wanaopinga utumiaji wa matangazo ya kimtandao kwa ajili ya siasa wanaona inaweza kutumiwa vibaya kwa ajili ya kupotosha kundi au aina ya watu flani tuu..
Katika uchaguzi wa 2016 Facebook walijikuta kwenye skendo kubwa baada ya kuonekana kuna vikundi vya kijasusi vya mataifa mengine vilivyoweza kutengeneza matangazo na kurusha kwenye mtandao wa Facebook kuwalenga wamarekani na kumpigia kampeni zaidi Rais Trump.

Teknolojia ya matangazo ya mtandaoni ina nguvu kubwa sana katika kupata data zinazohusu aina ya watu unaotaka kuwafikia. Hii ni nguvu kubwa ya kiteknolojia ambayo haipatikani katika mifumo mingine yeyote ya kimatangazo kama vile redio, tv, mabango na magazeti. Suala hili wengi wanawasiwasi litatumika vibaya mbeleni kwani kuchuja matangazo ya kimtandao si jambo rahisi.