Mauzo ya simu za iPhone 16 zilizozinduliwa hivi karibuni yameonesha kuwa ya chini kuliko ilivyotegemewa. Kupitia data/takwimu za mauzo ya awali (preorder), na data zinazohusu uzalishaji na usafirishaji wa simu hizo, watafiti wameona picha isiyonzuri kwa mauzo ya simu hizo kwa mwaka huu.

Kuna simu milioni 37 za iPhone 16 (hii ikujumuisha na matoleo ya Pro) zilizoagizwa hadi mwisho wa wiki ya kwanza ya kuanza kupatikana, hii inawakilisha upungufu wa asilimia 12.7 ikilinganishwa na idadi ya simu za iPhone 15 zilizouzwa kufikia mwisho wa wiki ya kwanza mwaka jana.
Lakini hii inamaanisha nini kwa Apple na sekta nzima ya simu za mkononi?
Ukomavu wa Matoleo ya Kawaida dhidi ya Pro: Wakati iPhone 16 na iPhone 16 Plus zimenunulika zaidi kwa asilimia 10% na 48% ukilinganisha na matoleo ya iPhone 15 katika kipindi hicho, matoleo ya 16 Pro na 16 Pro Max hayajafanya vizuri. iPhone 16 Pro imepungua kwa kiwango cha 27% na Pro Max kwa 16%. Hii inaonesha mwelekeo mpya wa wateja kuona bado matoleo ya kawaida ya bei nafuu yana thamani kubwa kuondoa haja ya kuingia gharama kubwa ili kupata matoleo ya Pro.
Ukomavu wa Soko: Kushuka kwa idadi ya oda kwa ujumla wake kunaweza onesha upungufu wa wateja wapya huku wale wa zamani wakiona hakuna kipya kwenye matoleo haya mapya cha kuwalazimisha kununua. Na hii inaweza kuwa sababu muhimu kwani kuna maboresho machache katika matoleo haya, nje ya ujio wa utumiaji wa Akili Mnemba (AI) ulioboreshwa hakuna jipya sana katika matoleo haya. Uwezo wa Akili Mnemba ya Apple Intelligence uliotambulishwa, bado haupatikani. Utakuja baadae kupitia masasisho ya iOS, inawezekana kuna wanaosubiri hilo kwanza.
Hali ya Kiuchumi: Hali ya uchumi wa dunia pia inaonekana kuchangia kwenye kuathiri maamuzi ya matumizi ya wateja. Mfumuko wa bei, ukosefu wa uhakika kiuchumi, na gharama kubwa za simu hizi za hali ya juu zinaweza kuwafanya wateja wawe waangalifu zaidi kuhusu kubadilisha simu zao. Katika mazingira ya sasa ya kiuchumi, watu wanatazama kwa umakini zaidi thamani wanayoipata kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi wa vifaa vya gharama kubwa kama simu za mkononi – hasa kama walizonazo bado wanaona zinakidhi mahitaji yao.
No Comment! Be the first one.