Mauzo ya kompyuta 2020 yapo juu, Data za kimauzo kutoka shirika la tafiti za masoko la Canalys zinaonesha kuna jumla ya kompyuta milioni 79 ziliuzwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka huu (Julai – Septemba 2020).
Janga la COVID19 – Korona lililosababisha watu wengi wafanyie kazi majumbani limechangia katika ukuaji huu wa mauzo wa kompyuta. Na mauzo haya yanaonekana ni habari njema kwa kompyuta zinazotumia programu endeshaji ya Chrome OS, zinazofahamika kwa jina la Chromebooks.
Mauzo ya kompyuta milioni 79 ni ukuaji wa asilimia 12.7 ukilinganisha na mauzo ya kipindi kama hicho mwaka jana, yaani Julai hadi Septemba 2019.
Katika mauzo hayo vifaa vya kompyuta kwenye makundi ya ‘notebooks’, yaani laptop pamoja na tableti ndizo zilizouzika zaidi. Hizi zilichangia mauzo ya milioni 64 kutoka kwenye ile jumla ya vifaa milioni 79 vilivyouzwa. Idadi inayobaki ambayo ni asilimia 28.3 ni ya uuzaji wa kompyuta kubwa – za mezani.
Makampuni yanayoongoza kimauzo: Lenovo, HP na Dell wanaoshikilia nafasi tatu za juu kimauzo – ndio wote kwa pamoja wameuza asilimia 65.4 ya hizo kompyuta milioni 79.
Lenovo anashikilia nafasi ya kwanza kwa kuuza vifaa milioni 19, HP nafasi ya pili kwa kuuza kompyuta milioni 18.6 na huku Dell akiuza kompyuta milioni 11.9. Lenovo na HP wote wana ukuaji wa mauzo wa zaidi ya asimilia 10 kila mmoja ukilinganisha na mauzo ya mwaka jana, huku Dell mauzo yakiporomoka kwa asilimia 0.5.
Chrome OS ni programu endeshaji ya kisasa inayotengenezwa na Google. Tayari makampuni mengi kama hayo niliyoyataja hapo juu yanatengeneza laptop zinazokuja na programu endeshaji ya ChromeOS. Bila kujali watengenezaji wa laptop husika, laptop zinazotumia programu endeshaji ya ChromeOS huwa zinapewa jina la Chromebook.
Laptop za familia ya Chromebook nazo zinaendelea kuonesha ukuaji wa kasi katika mauzo yake. Kwa ujumla Chromebooks milioni 9.4 ziliuzwa katika kipindi cha Julai – Septemba mwaka huu, huu ukiwa ni ukuaji wa mauzo wa asilimia 122 ukilinganisha na mauzo ya mwaka jana kipindi kama hicho. Katika kipindi hicho cha miezi mitatu HP aliuza Chromebooks milioni 3.2, huku Lenovo naye akiuza laptop za Chromebooks milioni 1.8 – kwa Lenovo idadi hiyo ni ukuaji wa asilimia 300 ukilinganisha na mauzo yao ya Chromebooks katika kipindi kama hicho kwa mwaka jana.
Wezesha bando kwa kutuma kiasi chochote kupitia Selcom, kwenye simu yako bofya *150*50*1# kwenye namba ya malipo weka 60751369 jina litakuja TEKNOKONA.
Mbunifu na mpenda teknolojia.
Muanzilishi wa Teknokona, TechMsaada na Teknokona Group LTD - WWW.TEKNOKONAGROUP.COM
Muda wangu umegawanyika kati ya kazi kibunifu @teknokonagroup na uandishi wa habari za Teknolojia hapa Teknokona Blog.
| mhariri(at)teknokona.co.tz |
No Comment! Be the first one.