Mauzo ya PS5 ya Sony yazidi kupanda. PS5 inaendelea kufanya vizuri sokoni. Kifaa hichi spesheli kwa ajili ya upatikanaji na uchezaji wa magemu kimekuwa sehemu muhimu ya mapato ndani ya kampuni ya Sony.
Katika mwaka wa mapato wa Sony ulioishia Machi 31, 2023 (ulianza April 2022), Sony wameonesha walipata mapato ya yen (pesa ya Korea Kusini) Trilioni 1.21, sawa na Dola bilioni 8.9 za kimarekani – ambayo ni zaidi ya Tsh Trilioni 20. Mapato haya ni asilimia 10 ukilinganisha na kipindi cha fedha cha kampuni hiyo kilichopita.
Ingawa mauzo yamechangiwa na bidhaa nyingi za kisasa zilizo kwenye familia ya Sony, Sony wamekubali ya kwamba PS5 kupitia mauzo ya Playstation 5 milioni 19.3 (ukilinganisha na milioni 11.5 kwa mwaka wa kabla) yamechangia sana mapato kwao.
Kwa mwaka wa fedha mpya Sony wanategemea kuuza zaidi ya PS5 milioni 25.
Soko la magemu kwenye PS5 liliuza magemu milioni 107.8, hii ikiwa ni ukuaji wa kutoka milioni 67.2 kwa mwaka uliopita.
Mambo si mabaya pia kwa mshindani wake, Microsoft kupitia Xbox Series X|S aliuza Xbox milioni 14.6 katika kipindi hicho, hii ikiwa ni ukuaji – kutoka mauzo ya Xbox milioni 8.7 katika kipindi kilichopita.
Kwenye soko la utengenezaji na uuzaji wa TV kampuni hiyo imeendelea kuona kuporomoka kwa mauz0 kutokana na ushindani mkubwa kutoka makampuni mengine hasa hasa ya kutoka nchini China. Pia maeneo mengine kama vile kwenye kitengo cha filamu pia hawakufanya vizuri kimauzo.
Kitengo cha magemu kupitia huduma ya PS5 kinategemea kuendelea kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Sony. Huku huduma kama zile za malipo ya kila mwezi (subscription) huku wateja wakipatiwa uwezo wa kucheza maelfu ya magemu zinategemewa kuendelea kuongeza mapato endelevu kwa kampuni hiyo.
Kama ulikuwa haufahamu, sekta ya magemu inaingiza mapato mengi zaidi ulimwenguni kote ikiipiku sekta ya filamu na muziki. Mfano kwa mwaka 2022, sekta ya magemu iliingiza mapato ya dola bilioni 332.4, huku muziki ikiingiza dola bilioni 20.9 na filamu ikingiza dola bilioni 19.5 (Kumbuka dola bilioni 1, ni sawa na Tsh Trilioni 2.4).
Ingawa Sony inajishughulisha na biashara nyingi katika sekta ya vifaa vya elektroniki na starehe, inaonekana bado biashara yao za magemu inaweza kuendelea kuwa kitengo muhimu sana katika utengenezaji wa faida katika kampuni hiyo.
No Comment! Be the first one.