Magari kuuzwa ni jambo la kawaida, ila fikiria kununua gari moja kati ya 64 tuu yaliyowahi tengenezwa…tena kwa ubunifu wa hali ya juu kiasi la kuyafanya kuwa tofauti zaidi na mengine. Na hii ndio sifa ya McLaren F1.
Magari ya familia ya McLaren F1 yalitengenezwa 64 tuu kati ya mwaka 1993 hadi 1998, lakini jamii ya McLaren F1 ya gari linalouzwa na McLaren kwa sasa ni lililotengenezwa mwaka 1998, na katika mwaka huo yalitengenezwa sita tuu.
Gari hilo ni jepesi ila lenye parts zenye ugumu unaoitajika, teknolojia ya kisasa ya carbon fiber ilitumika katika utengenezaji wake. Lina siti mbili za abiria ambao wanakaa upande wa kulia na kushoto wa dereva.
Wakati huo kadhaa yaliuzwa kwa watu binafsi lakini hili moja likawekwa kwenye kumbukumbu za McLaren, wakilitunza na kulifanyia service chini ya timu yao ya MSO (McLaren Special Operations). Kwa sasa gari hilo linaonekana lishatembea kilomita 4506, kiasi ambacho ni kidogo sana na hivyo ni kama gari mpya kabisa.
Bei bado haijawekwa wazi ila inaonekana gari hilo litauzwa kwa bei ya juu sana na kuna uwezekano mkubwa itanunuliwa na matajiri wapenda magari.
Vyanzo: Forbes na mitandao mbalimbali