Mwezi huu wa 12, huduma ya SMS imefikisha miaka 25. Hii ni tokea SMS ya kwanza kutumwa, ilitumwa mwezi wa 12, tarehe 3 mwaka 1992 huko nchini Uingereza.
Ujumbe huo mfupi ulitumwa na kijana wa miaka 22, Bwana Neil Papworth wa kampuni ya utengenezaji programu za kompyuta ya Sema Group, na alituma ujumbe huo kwenda kwa Bwana Richard Jarvis – ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mkurugenzi katika kampuni ya Vofafone ya huko nchini Uingereza.
SMS hiyo aliituma kwa kutumia kompyuta na ilipokelewa na Bwana Richard aliyekuwa anatumia simu ya Orbitel 901.
Ujumbe mfupi huo wenye sifa ya kuwa wa kwanza duniani ulisomeka ‘Marry Christmas’ – Heri ya Sikukuu ya Krismasi.
Kikubwa kufahamu ni kwamba kwa muda huo bado teknolojia hiyo ya SMS haikuruhusu simu kutuma, bali zilikuwa na uwezo wa kupokea tuu na ndiyo maana ujumbe uliandikwa na kutumwa kutoka kwenye kompyuta.
Kingine cha kufahamu:
Siku hii ambayo kijana alituma ujumbe huu mfupi: Nyimbo ya Whitney Houston ‘I will always love you’ ilikua juu kwenye chati Marekani na nchi zingine mbalimbali, pia filamu ya Home Alone 2 nayo ilikua ipo juu kwenye chati ya mauzo kwenye majumba ya sinema.
Mwaka mmoja baadae baada ya tukio hili la SMS ya kwanza kutumwa, nchi ya Finland ndio ikawa taifa la kwanza kuwa na mtandao wa simu ulioanzisha huduma ya kutuma na kupokea SMS kwa wateja wake. Kampuni ya Nokia ya nchini humo ndio ikawa kampuni ya kwanza kuanza kuingiza sokoni simu zenye uwezo wa kutuma na kupokea SMS.
Kuna SMS bilioni 20 zinatumwa kila siku duniani kote, wakati ujumbe wa kuchati unaotumwa kupitia Facebook Messenger na WhatsApp ni zaidi ya bilioni 60 kwa siku! – Facebook.
Ukuaji wa huduma na utumiaji wa huduma hiyo ulichukua miaka mingi sana, mfano kwa mwaka 1995 kwa kila mtumiaji wa simu ya mkononi alikuwa na wastani wa kutuma ujumbe wa SMS 0.4, yaani karibia SMS moja kwa watumiaji wawili. Hii ni ndogo sana. Sababu kubwa ilikuwa pia haikuwa inawezekana kwa watumiaji wa mitandao tofauti ya simu kutumiana ujumbe mfupi (SMS). Mfano kwa Uingereza hili liliwezekana mwaka 1999.
Pia katika mataifa mengine kama Marekani huduma hii ilianza kupata changamoto kwa kuwa ilikuwa bei ghali na wakati muda huo huduma za kuchati za kimtandao zilikuwa maarufu nchini humo.