Microsoft ni moja ya makampuni makubwa ya teknolojia duniani, Microsoft 4Afrika Initiative ni mpango wao wa maendeleo unaochochea ukuaji na utumiaji wa teknolojia, ubunifu na ujuzi.
Programu hii spesheli ya Microsoft 4Afrika Initiative ilianzishwa rasmi mwezi wa pili mwaka 2013. Lengo kuu likiwa ni kusaidia ukuaji wa haraka wa uchumi wa bara la Afrika kupitia kuimarisha uwezo wa kiushindani kupitia upatikanaji wa teknolojia kwa gharama nafuu, pia kupitia ubunifu na ujuzi wa hadhi ya kimataifa.
Kimombo – Affordable access to technology, Innovation & World class skills
Microsoft 4Afrika inahusisha juhudi mbalimbali, baadhi ya programu zilizochini ya mpango huu wa Microsoft 4Afrika ni pamoja na i) Upatikanaji wa teknolojia, ii) masuala ya ubunifu, na iii) ukuzaji wa ujuzi wa kiwango cha juu.
Upatikanaji wa teknolojia
Katika eneo hili Microsoft wanasaidia juhudi za upatikanaji wa teknolojia kwa gharama nafuu. Hii hujumuisha vifaa mbalimbali na teknolojia kama Cloud.
Teknolojia za kisasa kwa sasa ni muhimu katika utendaji wa kazi na utoaji wa huduma mbalimbali za kisasa. Iwe maeneo ya utoaji wa huduma za kijamii, biashara ata viwandani, utumiaji wa teknolojia uboresha shughuli nzima inayofanyika.
Kupitia programu ya Microsoft 4Afrika Initiative – Microsoft wanasaidia katika usambazaji wa vifaa janja vya familia ya Windows, hii ikiwa ni pamoja na kompyuta na simu kwa vijana wa Afrika.
Pia kuna programu waliyoianzisha tayari nchini Kenya iliyopewa jina la Mawingu ambayo inahusika na usambazaji wa huduma ya intaneti kwa maeneo yasiyofikiwa na huduma hiyo kwa sasa.
Ubunifu wa kiteknolojia
Katika eneo hili Microsoft inasaidia juhudi za ubunifu na utengenezaji wa apps kutoka bara la Afrika na pia kwa ajili ya watumiaji wa Afrika.
Baadhi ya mambo yanayofanyika ni pamoja na uungaji mkono watengenezaji (developers) wa apps na programu kwa ajili ya programu endeshaji ya Windows – kwa ajili ya kompyuta na simu zinazotumia Windows.
Inasemekana wapo watu wengi barani Afrika wenye mawazo makubwa ya utengenezaji apps kwa ajili ya kutatua kitu flani lakini tatizo linakuwa hawana muda na uwezo wa kumudu gharama za mahitaji ya kiteknolojia yanayohitajika katika utengenezaji huo.
Masuala ya Ujuzi (Skills)
Katika eneo hili Microsoft wanafanyia kazi mpango wa kutengeneza mfumo wa elimu wenye hadhi ya kimataifa utakahusisha upatikanaji wa elimu kupitia mtandao (online) na pia nje ya mtandao.
Hii yote ikiwa ni kusaidia vijana wa Afrika kuweza kuwa na ujuzi mkubwa wa kujiajiri na pia kuweza kuwa na ujuzi utakaoweza kuwasaidia katika ushindani mkali uliopo katika soko la ajira.
Tayari katika eneo hili Microsoft wameanzisha Afrika Academy ambao ni mpango utakaowapa nafasi wahitimu wa elimu ya juu, viongozi serikalini na wadau wengine kuweza kupata ujuzi wa kisasa zaidi wa kiteknolojia.
Kwa muda mrefu bara la Afrika tumekuwa nyuma kwa kiasi kikubwa katika eneo la ujuzi wa kiteknolojia na ubunifu lakini ni kupitia juhudi kama hizi ndio maendeleo yanazidi kukua katika eneo la teknolojia.
Kwa sasa hakuna ubishi ya kwamba kazi nyingi na majukumu mengi ya kila siku yanahusisha utumiaji wa teknolojia au vifaa vya teknolojia kila siku.
Juhudi za Microsoft 4Afrika Initiative ni mfano mzuri unaonesha jinsi makampuni makubwa yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiteknolojia.
Chanzo: Mtandao wa Microsoft 4Afrika