Hivi karibuni tuliandika kuhusu Microsoft kuacha kutumia jina la Nokia katika simu mpya za Lumia zinazotumia programu ya Windows – (Soma – Microsoft Yaacha Jina La Nokia Katika Simu-Janja Za Lumia!) na wiki hii kampuni ya Microsoft imefanikiwa kuja sokoni na simu mpya ya Lumia iliyopewa jina la Microsoft Lumia 535.
Je kwa nini Microsoft wameacha kutumia jina hilo?
Katika mkataba wa manunuzi ya kitengo cha biashara za simu za Nokia kampuni ya Microsoft imepata kibali cha kulitumia jina la Nokia kwa miaka 10 kibiashara na baada ya hapo kampuni mama ya Nokia itakuwa huru kujiingiza kwenye biashara ya utengenezaji simu tena kupitia jina la Nokia. Kwa sasa kwa kipindi cha miaka kumi kampuni hiyo iliyojiwekeza kwenye mabiashara mengine makubwa katika teknolojia ya mawasiliano haiwezi kutengeneza simu za mkononi na kuziuza kwa kutumia jina la ‘Nokia’.
Hivyo kwa sasa kinachofanywa na Microsoft ni maandalizi mazuri ya kuacha kutumia jina hilo taratibu.
Microsoft Lumia 535 inakuja na matoleo mawili, moja litakuwa la laini moja na lingine la laini mbili. Mnunuaji atapata nafasi ya kuchagua.
Je ina sifa gani?
- Kioo – Inchi 5 (960 x 540pixels)
- RAM – 1GB
- Diski Uhifadhi -GB 8 pamoja na nafasi ya kuongeza ukubwa huo kupitia kadi za memori za ukubwa hadi GB 128
- Prosesa ya 1.2 GHz Snapdragon
- Mfumo wa mawasiliano wa 3G
- Programu Uendeshaji – Windows 8.1
- Batri ya Uwezo wa 1905mAh
- Kamera ya Mbele na Nyuma – 5 Megapixel
Bei ya simu hii inalenga watumiaji wa kawaida katika masoko kama ya India, na nchi zingine zinazoendelea zaidi kwani kwa sifa zake ni simu yenye uwezo wa saizi ya kati. Na hali hii inaonekana kwenye bei pia, kwani simu hii inatarajiwa kuuzwa kwenye dola 130 za kimarekani (Tsh 225,000) kabla ya kodi, na inategemewa kupanda kidogo baada ya kodi.
Je ushawahi kutumia simu za Lumia? Unapendezwa na nini hasa? Zungumza nasi kupitia akaunti zetu za Twitter, Instagram au Facebook.
No Comment! Be the first one.