Microsoft na Facebook waunganisha nguvu katika utengenezaji wa mkongo wa kusafirisha data za huduma ya intaneti unaounganisha bara la Amerika na Ulaya. Tayari kuna mikongo mingine ila huu unakuwa wa kwanza kuunganisha Marekani na Kusini mwa Ulaya.
Waya wa mkongo huo utaunganisha mji wa Virginia Beach katika jimbo la Virginia na mji wa Bilbao wa nchini Uhispania. Kutoka Uhispania mkonge huo utaunganisha na mikonge mingine inayenda sehemu zingine za Ulaya na mabara ya Afrika, na Asia.
Mkongo huo wa data utakuwa na urefu wa takribani Kilometa 6,600 na umepewa jina la MAREA, ujenzi utaanza mwezi wa nane na kukamilika mwakani mwezi wa kumi. Utakuwa na uwezo wa kusafirisha data kwa kasi ya hadi TB 160 kwa sekunde!
Kwa nini Facebook na Microsoft wawekeze katika mkongo huu?
- Wote wanaofisi zenye data za huduma zao katika eneo la Virginia na jirani ya hapo.
- Huduma zao zinauhitaji mkubwa wa usafirishaji data kutokana na watu wengi wanaotumia huduma zao mtandaoni
- Kutengeneza mkongo unaounganisha moja kwa moja kwenye vituo vyao vya data kuna hakikisha kasi inakuwa kubwa ya usafirishaji ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwanzo.
- Kwa sasa vituo vyao vya data hivyo usafirisha data umbali mrefu hadi New York na kisha kuunganishwa kwenye mikongo mingine ndio kuelekea bara la Ulaya.
‘Kila tunapobofya kwenye tovuti mbalimbali na kufungua mitandao huwa kuna kuwa na usafirishaji mkubwa wa data kutoka sehemu zilipohifadhiwa na kufunguka kwenye vivinjari (browser) vyetu’
Kutokana na Microsoft na Facebook kumiliki huduma ambazo zinawatumiaji wengi sana wamejikuta gharama za kusafirisha data zao zikizidi kupanda na hivyo wakaona si mbaya kuzidi kujihakikishia usalama wa huduma zao kwa kuwekeza katika njia nyingine za usafirishaji huo wa data.
Ukiondoa wenyewe ambao ndio waliokuja na mradi huo wamemuingiza mshirika wa tatu atakayehusika na kusimamia biashara yote ya mkongo huo huku akihakikisha data za Microsoft na Facebook ndio zinapewa kipaumbele. Kampuni ya mawasiliano Telxius (tawi la Telefónica) ya nchini Uhispania itahusika na usimamiaji mzima wa mkongo huo.
Vyanzo: Wired.com na vyanzo mbalimbali