Microsoft imeomba radhi baada ya kuajiri wasichana wacheza shoo ambao walikua wamevalia kama wanafunzi wa shule. Wacheza shoo hao walialikwa kutumbuiza katika mkutano wa watengenezaji wa magemu uliofanyika San Fransisco.
Microsoft waliajiri kikundi cha wacheza shoo ama dancers kwa ajiri ya kuburudisha katika tukio/tafrija baada ya mkutano wa watengenezaji wa magemu, wacheza shoo hao walivalia mavazi ya wasichana wa shule yaliyofupishwa zaidi kuonesha maumbile ya ndani ya wadada hao.
Tukio hilo liliwakasirisha sana wanaharakati wa usawa kwa wanawake ambao walisema kwamba kitendo hicho ni cha udhalilishaji wa utu kwa watoto wa kike. Inaaminika kwamba baadhi ya wageni katika tafrija hiyo walipeleka malalamiko yao kwa Microsoft.
Microsoft wanasema walikosea sana kuandaa tafrija ambayo wacheza sho wakike walivaa mavazi ambayo hayakuwasitiri ipasavyo.
Zaidi ya hayo makamu wa rais wa rasilimali watu (Human Resource) aliwaandikia barua pepe wafanyakazi wote na kuwaambia kwamba uongozi umesikitishwa na kushangazwa baada ya kuona picha za wanawake katika mavazi ya wasichana wa shule katika tafrija iliyodhaminiwa na Microsoft, aidha katika barua pepe bosi huyo amewaambia wafanyakazi kwamba ile sio namna ambavyo kampuni hiyo inawatendea wanawake na pia sio namna ambayo Microsoft inatakiwa iwakilishwe. Mwisho kabisa alimaliza kwa kusema kwamba timu ya uchunguzi ya ndani inaliangalia swala hilo ili kuelewa nini hasa kilitokea.
Huu ni mfano wa matukio ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma harakati za kupata usawa wa mwanamke, Teknokona tunaungana na wanaharakati wa haki za wanawake na watoto duniani kupinga unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto wa kike duniani kote.
Chanzo: Geekwire na mitandao mingine