Toleo lijalo baada ya Windows 8 litakuwa Windows 10 na si Windows 9! Haya yamesemwa leo huko jijini Francisco katika utambulisho rasmi wa toleo lijalo la programu uendeshaji maarufu duniani kutoka Microsoft. Wengi hawakutegemea hili! (Soma –Microsoft Kutambulisha Windows 9 Jumanne Hii!)
Cheryl Tunt kutoka kitengo cha mahusiano (PR) amedai majaribio ya Windows 9 ya ndani yalienda vizuri sana na uamuzi ukafanyika wa kufanya maboresho zaidi na kwenda moja kwa moja Windows 10…na hii ndiyo itakayoingia sokoni. Naye rais msaidizi katika kitenge cha programu-uendeshaji (OS) Bwana Terry Myerson alidai toleo hili la Windows 10 ni zuri sana na “haitakuwa sahihi kuliita Windows 9”.
Je ni nini kimebadirika?
Programu moja ya uendeshaji kwa ajili ya vifaa vyote!
Microsoft wamesema Windows 10 itatumika kama programu ya uendeshaji katika vifaa mbalimbali kama vile kompyuta, simu, tableti na hata vifaa vinginevyo vitumiavyo mawasiliano ya intaneti (Internet of Things). Windows 10 itaweza kujibadili na kuweza kujiweka sawa kulingana na kifaa inapotumika, pamoja na sifa hii kutakuwa na soko moja tu la programu/Apps (App Store) kwa ajili ya programu zote iwe kwenye simu, tableti au kompyuta. Mfumo wa kupata mabadiliko ya program-uendeshaji (OS Updates) na zile za apps/programu nazo zitapitia kwenye soko hilo.
‘Start Menu’ inarudi
Tulisema kuhusu hili. Kuondolewa kwa ‘Start Menu’ kwenye ujio wa Windows 8 hakukuwapendeza watu wengi sana na inaonekana Microsoft wamejifunza kutokana na makosa na sasa wanarudisha sehemu hiyo. Na zaidi ya yote ‘Start Menu’ inarudishwa ikiwa imefanyiwa maboresho kadhaa ikiwa ni pamoja na kukupa mtuamiaji uwezo wa kutafuta mafaili ya kwenye kompyuta na mambo ya kwenye mtandao/intaneti bila ata ya kufungua programu za kuperuzi kama Firefox na Chrome. Pia kupitia ‘Start Menu’ hii muonekano wa baadhi ya programu utakuwa kama ule wa kwenye Windows 8 maarufu kwa jina la ‘Tiles’, ikiwa ni mpangilio wa ‘kimraba kimraba’ (tazama picha), ila utakuwa na uwezo wa kubadilisha ukubwa wa vitu vinavyoonekana.
Apps/Programu zilizotengenezwa kwa ajili ya simu za mguso na tableti kufanya kazi ata kwenye kompyuta.
Katika kuzidi kuonesha maana ya programu moja ya uendeshaji kwa ajili ya vifaa vya aina zote apps zilizotengenezwa kwa ajili ya vifaa vya mguso (Touch) kama simu na tableti za Windows 8 zitaweza kufanya kazi kwenye kompyuta huku mtumiaji akitumia ‘Keyboard’ na ‘Mouse’ tuu katika utumiaji huo.
Sasa Fanya Kazi Nyingi kwa wakati mmoja bila usumbufu (Multitask)
Windows 10 imeboreshwa zaidi katika uwezo wa kupanga programu mbali mbali unazotumia kwa wakati mmoja. Hii ikiwa na kuboresha uraisi wa wewe kuhama kutoka programu moja hadi nyingine.
Itakuja lini?
Windows 10 inategemewa kuwa tayari kuingia sokoni ifikapo miezi ya kati mwakani (2015)
Kwa sasa ni hayo tuu. Kutoka sasa hadi pale Windows 10 itakapokuwa tayari kwa ajili ya kuingia sokoni tunategemea mabadiliko mbali mbali yatafanyika, endelea kutembelea Teknokona na hutapitwa. Kumbuka kuungana nasi kupitia akaunti zetu za Google+, Facebook na Twitter
Je unasubiria Windows 10 kwa hamu? Ni nini kinakuuzi zaidi kuhusu Windows 8?
Kilichonikera kwenye windows 8 ni kutokuwepo kwa start menu na wireless adapter