Baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa wasukaji wa programu, Safaricom, kampuni ya simu ya nchini Kenya iliyoleta M-pesa kwa walimwengu imetangaza kuachia nyenzo za kuunganisha programu binafsi (‘API’ ) kwenye mfumo wao wa M-pesa. Hatua hii inafungua milango mipya kwa ajili ya wabunifu kote duniani kuingiza M-pesa kirahisi na kwa njia tofauti kwenye mifumo ya biashara zao.
Hatua hii imewezekana baada ya Safaricom kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo wao wa M-Pesa na kupelekea mfumo huo kufikia hatua ya kuitwa toleo la pili lililopewa jina la M-Pesa G2. Toleo la kwanza, G1 liliweza kupata mafanikio makubwa katika nchi zinazoendela kuanzia Kenya, kusambaa barani Afrika na hata kufika nchi za bara la Asia.
Toleo hilo liliwezesha malipo ya papo-kwa-hapo kwa kutumia mfumo wa ‘Instant Payment Notification (IPN)’. Hatahivyo, ili kuiwezesha IPN kwenye malipo yasiyo ya kawaida ilibidi hatua za ziada zifanyike ili kufanya malipo. Kutokana na matumizi ya M-Pesa kukua na fursa zake kuongezeka, imebidi adha hii kurekebishwa kwenye toleo jipya la G2.
M-Pesa yaja Nyumbani
Inaripotiwa kwamba kwa muda mrefu, mfumo wa MPesa ulikuwa una makao yake katika nchi ya Ujerumani. Safaricom walifanikiwa mnamo amwezi Aprili, kuuhamisha kutoka huko na kuuleta karibu zaidi na watumiaji wake wa Kenya na Afrika kwa ujumla. Mkurugenzi wa idara ya huduma za Fedha wa Safaricom, Bi. Betty Mwangi alisema kwamba moja ya faida ya kuleta M-Pesa Afrika ni ukweli kwamba sasa itakuwa ni rahisi kwa ku-iunga na biashara nyingine ili kutoa huduma zaidi au kuboresha huduma kwa wateja.
Gazeti la Daily Nation la Kenya linamkariri Bi Betty akisema pia, “Tunakubali kwamba ubunifu hauwezi kutoka kwetu pekee – inahitaji ushirikiano ili kupata ufumbuzi bora wa matatizo utakaobadili maisha yetu”
Ubunifu Zaidi
Wasaukaji wa programu wanategemewa kubuni njia mbalimbali zinazowezesha miamala ya mteja-kwa-biashara, biashara-kwa-mteja na biashara-kwa-biashara kwa ufanisi zaidi kwa kutumia mfumo mpya wa M-Pesa. Pia mfumo mpya wa M-Pesa utawaruhusu wasukaji kuhusisha mazingira ya kipekee ya biashara kwenye ulipaji na M-pesa, kama kodi mbalimbali zinazohusika na biashara. Mifumo ya zamani ya ‘Lipa kwa M-pesa itaendelea kuwepo na itafanya kazi sambamba na hizi njia mpya ikitegemewa kwa pamoja zitawezesha Afrika kuondokana na malipo ya fedha ya za noti na sarafu (‘cash’).
Biashara
G2 inafanya mambo mengi zaidi kurahisisha miamala ya biashara. Biashara na mashirika makubwa yamekuwa yakitumia MPesa kwenye huduma zao kama njia muhimu ya malipo. Kwa mujibu wa Safaricom, wafanyabiashara na wateja wategemee sasa, mfumo wa M-pesa kurahisisha kupata stakabadhi za malipo ya bidhaa na huduma muhimu. Mfumo huu mpya unakuja na usalama zaidi na njia mpya ya kuruhusu au kukataa malipo unaowezesha urahisi wa kurudisha nyuma malipo yaliyokosewa au malipo kwa huduma ambazo hazipo kwa muda husika. G2 ni salama zaidi ya mfumo uliopita.
Safaricom wamechukua hatua hii mpya kutokana na ushindani mkubwa unaokuja katika malipo ya dijitali na inaiweka M-Pesa katika sehemu nzuri katika kuiingizia kipato. Hakuna kikomo cha ubunifu unaoweza kutoka kwa watu kutoka kona zote za dunia. Ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi yanakuja kutokana na hatua hii mpya ya M-Pesa kutoka kwa Safaricom.
Chanzo: cryptocoinsnews, safaricom, Daily Nation.
No Comment! Be the first one.