Katika tukio lisilotarajiwa na lenye kutisha, Pagers (vifaa vya mawasiliano) zinazotumiwa na wanachama wa kundi la Hezbollah zililipuka kwa wakati mmoja katika maeneo mbalimbali ya Lebanon na Damascus, Syria.
Tukio hili, lililotokea tarehe 17 Septemba 2024, limesababisha vifo vya watu 16 na kujeruhi zaidi ya watu 2,800. Shambulio hili linaonekana kuwa la aina yake katika ulimwengu wa teknolojia na usalama.
Pager ni nini?
Pager ni kifaa cha mawasiliano kwa njia ya jumbe fupi na kwa sauti ambacho kinatumia teknolojia za zamani, za kabla ya ujio wa simu janja. Vifaa vya page vilianza kutumika miaka ya 1950 hadi mwishoni mwa miaka ya 1990, ambapo ujio wa simu za mkononi ulifanya matumizi yake kupotea.
Makundi ya Hezbollah yamekuwa yanatumia njia hii ya mawasiliano kwa kuwa ni salama zaidi dhidi ya ufuatiliwaji wa kidukuzi ukilinganisha na simu. Unaweza kudukua jumbe ila huwezi kuwa na uhakika aliyetuma yupo wapi kwa wakati huo, hii ni tofauti na simu ambazo zinatuma data kuhusu maeneo zilizopo.
Chanzo cha Shambulio
Inaripotiwa kuwa shambulio hili lilitekelezwa na Israel kupitia udukuzi wa vifaa vya mawasiliano vya Hezbollah – wenyewe Israel hawajatoa taarifa rasmi za kukataa au kukubali. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Israel ilifanikiwa kuingilia na vifaa hivyo, na kuvifanya vijilipuke kwa wakati mmoja. Hii ni mara ya kwanza kwa shambulio la aina hii kutokea, vifaa hivi vyote inasemekana vilibadilishwa miezi kama mitatu nyuma. Kuna wanaoamini udukuzi huu haukuwa wa kawaida, inawezekana vifaa hivyo vyote viliwekewa vibomu vidogo kabla ya kuingia Lebanon – kwamba inawezekana vifaa hivyo vilishaathiriwa kutokea kwa muuzaji.
Athari za Shambulio
Milipuko hii ilisababisha majeraha makubwa kwa wanachama wa Hezbollah na raia wa kawaida waliokwenye sekta zilizopewa vifaa hivyo pia. Wizara ya Afya ya Lebanon imewataka raia wote wanaomiliki Pagers kuzitupa mara moja.
Maoni na Matarajio
Shambulio hili linaonesha jinsi teknolojia inaweza kutumika kama silaha katika migogoro ya kisiasa na kijeshi. Ni onyo kwa makundi mengine ya kigaidi na serikali zinazotumia teknolojia za zamani za mawasiliano. Pia, linaibua maswali kuhusu usalama wa vifaa vya mawasiliano na umuhimu wa kuboresha mifumo ya usalama dhidi ya udukuzi.
No Comment! Be the first one.