Kampuni ya Millicom inayomiliki kampuni ya Tigo duniani kote imefanikiwa kununua asilimia 85 za umiliki wa kampuni ya Zantel. Tulishaandika kuhusu kampuni ya Zantel kuwa katika deni kubwa la muda mrefu na wamiliki wa asilimia 85 ya kampuni hiyo, Etisalat kutaka kuuza umiliki wao.
Kampuni ya Zantel inamilikiwa kwa asilimia 85 na kampuni ya Etisalat wakati asilimia 15 zilizobakia zinamilikiwa na serikali ya Zanzibar.
Tayari makampuni mengi pia yalikuwa yanataka umiliki huo, hii ikiwa ni pamoja na Vodacom, soma – Zantel KUUZWA! Vodacom na Tigo waitamani!
Katika makubaliano yao, kampuni ya Millicom italipa dola moja ya kimarekani ambayo ni takribani tsh 2,000/= kwa kampuni ya Etisalat na kuchukua umiliki wa asilimia 85 katika kampuni ya Zantel lakini pia Millicom itawabidi walipe deni lote la Zantel ambalo ni takribani Tsh Bilioni 159 kwa benki ya kijerumani – Deutsche Bank.
Millicom imesema kampuni ya Zantel itaendelea kufanya kazi kama kawaida na wao wanategemea kutumia teknolojia muhimu zinazomilikiwa na Zantel katika kuzidi kuboresha huduma zake hasa kwa Tigo. Tayari Tigo imeanza kuzidisha juhudi katika kusambaza teknolojia ya 4G na uamuzi huu kwa kiasi kikubwa utawasaidia sana kwani Zantel ndiye yenye umiliki wa huduma ya intaneti ya kasi inayoletwa na mkonge (Fibre) ya EASSy.
Ununuaji huu unasubiria baraka za TCRA tu kwa sasa ili kukamilika.
Je unamaoni gani juu ya ununuzi huu?
No Comment! Be the first one.