Google imetoa taarifa kuwa inaongeza muda wa kutoa maboresho mabalimbali kwa kivinjari chake cha Google Chrome kinachotumika katika programu endeshaji ya muda mrefu ya Windows XP. Maboresho hayo ni hadi mwishoni mwa mwaka huu tuu.
Taarifa hiyo inamaanisha kuwa Google watajikita tuu katika kutoa maboresho na ubora wa kiusalama katika kivinjari chao kwa miezi 8 zaidi kwa watumiaji wa Windows XP.
Google hapo mwanzo (2013) walisema kuwa wataacha kuboresha na kuongeza usalama katika kivinjari chao cha Chrome kwa programu-endeshaji ya Windows XP kufikia mwezi wa nne mwaka huu. Lakini taarifa mpya imetoka na inasema kuwa kampuni imeongeza muda kidogo hadi mwishoni mwa mwezi 2015
April 8, 2014, yaani mwaka mmoja uliopita ndio tarehe rasmi ambayo kampuni ya Microsoft iliachana na kutoa sapoti ya kimtandao, ya kimaboresho na ulinzi kwa programu endeshaji hii na wakaimiza watumiaji wote wahamie kwenye matoleo mapya kama vile Windows 7 na 8.
Kupitia blogu yao ya masuala ya ulinzi, afisa wao Bwana Mark Larson alieleza kuwa kutokana na kukosekana kwa maboresho ya usalama (security Updates) katika kompyuta zinazotumia Windows Xp zaidi ya mwaka mzima sasa, kompyuta hizi zipo katika hali tete na ambayo inaweza leta maafa makubwa sana kwa watumiaji wake kiusalama. Kwa kuwa Chrone inajikita zaidi katika kuhakikisha mtumiaji anatumia intaneti kwa kiwango cha juu chenye usalama ndani yake, kompyuta ambazo hazitumii programu-endeshaji ambazo zinapata maboresho ya kiusalama hazifai kwa sasa kwa kuwa ni rahisi sana kushambuliwa na virusi na hata ‘Malware’.
“Mamilioni ya watu bado wanatumia kompyuta zenye Windows XP kila siku. Tunataka hao watu wawe na chaguo la kutumia kivinjara kinachoenda na wakati na pia chenye usalama zaidi” – Alisema Mark Larson
Ukweli ni kwamba watumiaji wa Windows Xp ni wengi sana na inawabidi wabadilishe programu-endeshaji hiyo kwa kuwa ina tuhuma za kuwa rahisi kukumbwa na majanga kama yale ya kupata Virus kwa haraka.
Kulingana na taarifa zilizokusanywa na Net Applications, Windows Xp bado ni moja ya programu endeshaji inayotumika zaidi, inashikilia asilimia 16 kwa utumiaji duniani kote kwa data za mwezi uliopita, na hiyo ni namba kubwa kwa Programu-endeshaji ya mwaka 2001. Watumiaji wa Windows Xp wanaweza kupakua kivinjari cha Internet Explorer hadi toleo namba 8 wakati sasa kuna hadi Internet Explorer 11 ambayo inatumiwa na windows 8.
No Comment! Be the first one.