Ushawahi kuwaza jinsi ndugu na marafiki wa wafungwa wanavyohaha juu na chini kuwasaidia wafungwa hao? Hii ni moja ya vituko vilivyotokea huko jimbo la Carolina ya kusini, nchini Marekani.
Masalia ya ndege isiyoongozwa na rubani (yani, ‘drone’ kwa kiingereza) yamekutwa nje ya gereza moja linalolindwa kwa usalama wa hali ya juu kwenye jimbo la Carolina ya Kusini. Utawala wa gereza hilo umesema kuwa wanaamini ndege hiyo ilikuwa ikitumika kujaribu kusafirisha simu, bangi na tumbaku kuelekea gereza hilo liitwalo Lee Correctional Institution.
Shirika la habari duniani la Reuters linaripoti kuwa msemaji wa idara ya urekebishaji, Bi. Stephanie Givens alisema kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa ndege aina hiyo kutumika kuingiza simu au vitu vingine vilivyopigwa marufuku kwenye magereza ya jimbo la Carolina ya Kusini. Bi. Stephanie anaendelea kwa kusema, “Mara nyingi simu zinatupwa juu ya ukuta. Teknolojia inakuwa na sisi inatubidi kunatafuta njia tofauti za kukumbana nayo.”
Uchunguzi wa tukio hilo lililotekea April, mwaka huu unaendelea. Tayari, kijana Brenton Lee Doyle wa miaka 28 amekamatwa na mtu wa pili anayeshukiwa kuhusika na uhalifu huo anatafutwa. Kijana Brenton amekana kuona ndege yoyote maishani mwake na wakili wake amesema wala kijana huyo hakuambiwa na polisi kuwa alikuwa akikamatwa kwa kosa la kurusha ndege. Kesi hiyo inaendelea.
Kesi hiyo inayomuandama kijana huyo si ngeni. Mahali kadhaa duiani pameripotiwa kutumika ndege ndogo za kuongozwa bila rubani kwa uhalifu. Ingawa teknolojia hii imepokea umaarufu mkubwa kwa kutumiwa na jeshi la marekani, ndege hizo zimeanza kupatkiana kwa watu wa kawaida wenye fedha za kutosha. Nedege hizo zinaweza kupatikana kwa takribani dola za kimarekani 1000, yani million moja na laki sita za kitanzania. Ndege hizi zinatumika kwa madhumuni mengi kama uchunguzi, kuwasilisha bidhaa kwa wateja, kutengeneza sinema na hata kwa michezo. Je, wewe unasemaje kuhusu teknolojia hii? Ushawahi kufikiria kutumia teknolojia hii? Je, ni sahihi kuiita ndege isiyoongozwa na rubani? Tupe maoni yako!
Picha na AP.
No Comment! Be the first one.