Gmail ni njia nzuri zaidi ya kusoma barua pepe. Ukiachana na hili ndio njia ambayo inatumika na watu wengi katika kutuma na kupokea barua pepe zaidi duniani ukilinganisha na huduma zingine kama vile Yahoo.
Kama unavyojua baadhi yetu tuna vyanzo vingi sana vya kusoma barua pepe zetu. Vyanzo hivi viko tofauti tofauti sana kwa mfano mtu anaweza akawa na barua pepe ndani ya Gmail, Yahoo na hata Hotmail. Sasa kuwa na barua pepe katika sehemu zote hizi mara nyingine kunachosha maana itabidi ufungue moja moja na kuanza kupitia. Lakini vipi kama ungeweza kuzikusanya zote na kuzisoma katika Gmail?
Fuata Njia Hizi Kuliwezesha Hili:
KWANZA: Ingia katika akaunti yako ya Gmail
Njia ya kwanza kama kawaida ni kuingia katika akaunti yako ya Gmail, ukifika ndani nenda katika sehemu ya settings. Baada ya hapo nenda katika sehemu ya ‘Accounts and Import’ na kisha ingia katika eneo la ‘Add POP3 Email account’
PILI: Weka anuani ya barua pepe (E-mail) yako ya Yahoo, Hotmail au sehemu nyingine
Ukishabofya kwenye ‘Add POP3 email account’ ukurasa mpya utafunguka ambapo itakubidi uingize anuani ya barua pepe ambayo unataka kusomaea barua pepe zake ukiwa katika Gmail (Kwa mfano xxxx@hotmail.com). Cha muhimu hapa ni kwamba unaweza ukaongeza mpaka akaunti 5 za anuani ya barua pepe.
TATU: Weka taarifa zako za Yahoo, Hotmail au sehemu nyingine
Bofya ‘Next Step’ ili kuendelea kuingiza taarifa zako za muhimu zinazohusiana na barua pepe zako ambazo utakuwa unazisoma ukiwa katika Gmail. Hii inamaanisha ni kujaza taarifa za muhimu kama vile nenosiri n.k.
NNE: Hakikisha Taarifa zako
Ukishamaliza tuu kubofya ‘Add account’ baada ya kujaza taarifa zote za umuhimu, Gmail itaanza kuangalia barua pepe na kama ikipata yeyote basi unaweza ukaisomea humo humo (Gmail) bila ya kuingia katika Yahoo, Hotmail na sehemu nyingine.
TANO: Hakikisha Mabadiliko Yako
Hii ni njia ya mwisho, hapa inakubidi urudi katika Settings na kisha nenda katika ‘Account and Import’ ndani ya Gmail. Ukifika hapo chagua chaguo la ‘Send Mail From Another Address’. Ukifanya hivyo utakuwa na uwezo wa kutuma barua pepe za Yahoo, Hotmail na sehemu zingine ukiwa ndani ya Gmail.
Unaemtumia barua pepe hatajua unatumia Gmail kujibu barua pepe zake (kama alikutumia kupitia Yahoo, Hotmail na sehemu zingine). Mtumiaji ambae anaweza akaona kama umemjibu kupitia Gmail ni mtumiaji ambaye amekutumia barua pepe kupitia katika huduma ya Outlook. Kwa mtumiaji wa Outlook, mtumiaji huyo atakuwa na uwezo wa kuona kichwa cha barua pepe ambacho kitakuwa kinasomeka ‘Sent on behalf of xxxxx@gmail.com) yaani ‘imetumwa kwa niaba ya xxxx@gmail.com)
Ukiachana na hilo bado njia hii inakuwa ni nzuri sana, hebu fikiria kuzikusanya zote sehemu moja na kuweza kuzijibia hapo? Unataka nini tena?