Tarehe ya uuzwaji wa simu ya Nokia 3310 (2017) unazidi kukaribia kwa kasi, lakini habari mpya kuhusu simu hiyo kunaweza kuathiri uuzwaji wake katika baadhi ya nchi Duniani.
Nokia inatarajiwa kuuzwa kuanzia mwezi Mei mwaka huu.
Simu hiyo iliyotoka kwa mara ya kwanza mwaka 2000 na kuuzwa Takribani 126 milioni, ujio wake mpya umewafurahisha wapenzi wengi wa Simu za Nokia.
Pamoja na makala nyingi kuandikwa kuhusu ujio wake, Kwa mujibu wa mtandao wa Nokia simu hiyo ya 3310(2017) itakuwa na 2G Bands. Ujio huo mpya wa simu ya Nokia 3310(2017) unaweza kuingia dosari kwa baadhi ya nchi kutokana na simu hiyo kutumia Teknolojia ya 2G pekee, ambapo Frikwensi zake ni 900 MHz na 1800 MHz.
2G ni teknolojia iliyotamba sana miaka ya 1990 ambapo inamuwezesha mtu kupiga/kupokea simu, kutuma/kupokea ujumbe mfupi . Teknolojia ya 2G ambayo pia huitwa teknolojia ya SMS, pia huwezesha kutuma ujumbe wenye picha, ambao huitwa MMS (multimedia messaging service).
Teknolojia ya 2G kwa baadhi ya nchi tayari mfumo huo umeondolewa. Mfano nchini Australia kampuni ya Telecom Telstra imezima 2G tangu mwaka jana Desemba, ambapo Vodaphone ya Australia nayo wanataraji baadae mwaka huu kuzima 2G.
Japani kampuni za KDDI iliondosha 2G machi 2008, Softbank Machi 2010, NTT DOCOMO Aprili 2016.
Nchi za Canada, Singapore, Taiwan, Marekani na Switzerland tayari baadhi ya makampuni ya mawasiliano yamezima 2G.
Kwa nchi ambazo baadhi ya kampuni za Mawasiliano zimezima na zinazotaraji kuzima 2G itakuwa ngumu kwa wananchi wake kukubali kununua simu hizo kwa kuwa hazitaweza kufanya kazi.
Orodha ya baadhi ya kampuni na nchi ambazo zimeshaondosha 2G na zinazotaraji kuondosha angalia picha iliyo chini.
Hata hivyo pamoja na nchi kadhaa kuanza kuzima 2G kwa nchi za Afrika inaonekana bado Teknolojia ya 2G ina nafasi na itahitaji muda kuzimwa. Hivyo simu hiyo ya 3310(2017) ina nafasi ya kuuzwa zaidi kwa nchi za Afrika na zile ambazo bado Teknolojia ya 2G inaenedelea kutumika.
Kwa changamoto hii pengine Nokia wanaweza kubadili gia angani kwa kuboresha toleo hilo ili liweze kukidhi mahitaji ya wengi.
Nini maoni yako kuhusu changamoto hiyo ya Nokia 3310 (2017) kwa baadhi ya nchi ambazo zimeanza kuzima mfumo wa 2G.