Wiki iliyopita, kampuni ya Nothing ilizindua bidhaa yao ya pili, ikiwa ni simu, inayoitwa Nothing Phone 1. Simu hii ni mwendelezo wa juhudi za kampuni hiyo katika kutengeneza bidhaa ambazo zitafanya muunganiko wa kielektroniki kushindana na miunganiko ya bidhaa (Ecosystem) kutoka kampuni nyingine, hasa Apple ambao kwa sasa ndio wenye muunganiko bora zaidi kwa bidhaa zao.
Simu ya Nothing Phone 1 ina mwonekano mzuri, ikifanana kimuundo na matoleo ya hivi karibuni kutoka kampuni ya Apple, kasoro mambo machache kama kamera ya mbele kuwa pembeni, kutumia waya aina ya Type C pamoja na mwonekano wa nyuma kuwa tofauti na simu nyingine.
Simu hii ina skrini yenye ukubwa wa inchi 6.55 ikiwa na paneli ya OLED yenye uwezo wa kubadili kasi ya kuonekana kwa taarifa (Refresh Rate) kati ya 60 Hz na 120 Hz huku ikiwa na mwanga wa kutosha kutumika katika mazingira mbalimbali.
Inakuja ikiwa na Chipset aina ya Qualcomm Snapdragon 778G+, yenye uwezo wa 5G na pia kasi nzuri ya matumizi. Simu hii inatumia mfumo wa Android kutoka Google, ikija na mfumo wa Android 12 huku ukiwa na mwonekano wa Nothing OS, mwonekano ambao ni karibu kabisa na mwonekano mama kwa mifumo ya Android (Stock Android). Kamera katika simu hii ziko tatu, mbili zikiwa nyuma na moja ikiwa mbele. Kamera za nyuma zote zina uwezo wa Megapixel 50, sensa za kamera hizi zikitokea Sony na Samsung. Kamera ya mbele ina uwezo wa Megapixel 16.
Kivutio kikubwa katika simu hii, mbali na mwonekano wa kimfumo, ni mwonekano wake kimuundo, hasa nyuma ambapo kampuni ya Nothing imeamua kutumia kioo, lakini zaidi sana kutoweka rangi katika kioo hicho, kikiacha vifaa ndani ya simu hio kuweza kuonekana, japo vikiwa vimefunikwa kwa plastiki nyembamba katika rangi nyeupe ama nyeusi. Nyuma pia kuna mpangilio wa taa ndogondogo mia tisa, zilizobuniwa kutengeneza mwonekano wanaouita Glyph Interface, yaani mpangilio wa taa zinazoashiria vitu mbalimbali kuanzia kuchaji, simu zinazopigwa, jumbe hata kuweza kutumika kama taa ya picha na video. kuna taa nyekundu pia inayowaka wakati video inaporekodiwa.
Simu hii ina RAM ya GB 8 au 12, huku ikiwa na uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu wa GB 128 au 256.
Nothing Phone 1 ina betri yenye ukubwa wa 4500 mAh, ikiwa na uwezo wa kuchaji kwa waya kwa nguvu ya Watt 33, ikitumia dakika 30 kufikia asilimia 50 na dakika 70 kujaa. Pia, inaweza kuchajiwa bila waya kwa nguvu ya Watt 15 na uwezo wa kuchaji vifaaa vingine kwa nguvu ya Watt 5.
Simu hii inasapoti mawasiliano ya 5G huku ikiwa na huduma za WiFi 6 na Bluetooth 5.2. Ina teknolojia ya utambuzi wa alama za vidole, ikiwa haina sehemu ya kuchomeka earphones. Inatumia waya wa kuchaji na taarifa aina ya USB Type-C. Simu hii inapatikana katika matoleo mawili ya rangi, Nyeupe na Nyeusi.
No Comment! Be the first one.