Katika taarifa yao ya mapato waliyoitoa jana Facebook wametoa pia data zinazohusu utumiaji wa mtandao huo mkubwa duniani. Kufikia Novemba 2 tovuti hiyo imekuwa na wastani wa watumiaji bilioni 1.79 kila mwezi.
Watumiaji hawa ni wale ambao uingia katika tovuti hiyo angalau mara moja kila mwezi. Idadi hii ya bilioni 1.79, ni ukuaji wa asilimia 16 ukilinganishwa na wakati kama huu mwaka jana.
Tovuti inayojihusisha na data za kuhusu watumiaji intaneti duniani kote, Internet Live Stats, imekadilia ya kwamba kuna takribansi watumiaji bilioni 3.42 wa intaneti kufikia mwezi Julai mwaka 2016. Data za Facebook zinamaanisha takribani asilimia 52 ya watumiaji wote wa intaneti duniani wana akaunti kwenye mtandao wa Facebook (na wanafungua akaunti zao angalau mara moja kila mwezi).
Ukuaji wa watumiaji wa Facebook unauweka mtandao huo katika nafasi nzuri zaidi kibiashara. Tayari wanaingia mabilioni ya dola za kimarekani kila mwezi kutokana na matangazo yanayowekwa kwa watumiaji wake.
Ukuaji wa watumiaji wa huduma ya intaneti hasa hasa katika mataifa yanayoendelea kuna maanisha idadi ya watumiaji intaneti na wanaojiunga katika mtandao wa Facebook itaendelea kukua.