Kama umepakua programu ya QuickTime kutoka Apple kwenye kompyuta yako ya Windows unashauriwa kuiondoa mara moja.
Watafiti mbalimbali wa mambo ya kiusalama wa kimtandao wamegundua ni rahisi sana programu hiyo kutumika kuvamia data za kompyuta zako kwa sasa.
Tayari Apple walishatangaza kuacha kutoa masasisho (updates) kwa programu yao hiyo ambayo mara nyingi ilikuwa inakuja moja kwa moja pale unapotaka kupakua programu ya iTunes.
Ingawa programu ya QuickTime bado inaendelea kuwa na uwezo wa kufanya kazi ila ina ubovu wa kiusalama (security vulnerabilities) ambao ni hatari kwa data zilizokwenye kompyuta yako.
Kama una programu hiyo fuata hatua hizi kuiondoa kwenye kompyuta yako;
Kwa watumiaji wa Windows 10:
- Bofya ‘Start’.
- Chagua “Settings.”
- Chagua “System” na nenda eneo la “Apps and features.”
- Tafuta QuickTime kwenye orodha na kisha bofya “Uninstall.”
Kwa watumiaji wa Windows 7:
- Bofya ‘Start’.
- Chagua “Control Panel.”
- Chagua “Programs” na kisha chagua na kubofya “Programs and features.”
- Tafuta QuickTime kwenye orodha na kisha bofya “Uninstall.”
Inasemekana kwa sasa ni kwa kompyuta za Windows tuu, Apple wanaendelea kutoa masasisho ya programu hiyo kwa wale wanaotumia kwenye vifaa vyao kama vile kompyuta za Mac.
Ni muhimu kuhakikisha unakuwa na programu zinazopata masasisho (updates) mara kwa mara ili kuzidi kukuhakikishia usalama wa data zako. Endelea kutembelea TeknoKona
vyanzo: grahamcluley.com na mitandao mbalimbali