Je unachukua hatua gani pale ambapo hali ya hewa inazidi kuwa mbovu katika jiji lenye magari maelfu kila siku barabarani? Piga marufuku yale yaliyozeeka, ndio uamuzi uliochukuliwa na serikali ya jiji la Paris.
Inafahamika wazi ya kwamba injini za magari yaliyochakaa yanatoa zaidi gasi chafu ukilinganisha na magari mapya na ya kisasa zaidi. Na ni kutokana na hili ndio maana serikali ya jiji la Paris limeona uhamuzi huu ni muhimu katika kuboresha hali ya hewa ya jiji hilo mashuhuri.
Kuanzia tarehe 1 mwezi wa saba mwaka huu, magari yote yaliyosajiliwa kabla ya 1997 na pikipiki zilizosajiliwa kabla ya mwaka 2000 hazitakuwa na ruhusa ya kutumika katika jiji hilo katika katika siku za kazi (weekedays), yaani Jumatatu hadi Ijumaa.
Mpango huu ni endelevu na lengo kuu ni kuhakikisha ya kwamba itafikia sehemu magari yenye umri wa zaidi ya miaka 10 hayatakuwa yanaruhusiwa kutumika kabisa katika jiji hilo.
Jiji hilo limejipanga kupanga magari katika makundi kulingana na sifa zake kwa mazingira, magari kama vile yanayotumia umeme na yale yanayotumia ‘hydrogen’ badala ya mafuta yatakuwa ya daraja la kwanza – yaani rafiki wa mazingira.

Uamuzi kama huu ungechukuliwa katika mataifa kama yetu ya huku Afrika basi ungekuta ungeathiri zaidi ya asilimia 40% ya magari yote, lakini inasemekana kwa jiji la Paris ni takribani asilimia 10 tuu ya magari ndio yataathirika na uamuzi huu.
Ila asimilia 10 hiyo ya magari inasemekana inachangia zaidi ya nusu ya gesi chafu yote inayozalishwa kutoka kwenye magari yanayotumika katika jiji hilo.
Kuna wakazi wengi ambao wamekasirishwa na uamuzi huo wakisema ni hatua ambazo wanaoathirika ni watu maskini, ambao wanaitaji kutumia magari hayo kwenye usafiri kwenda kazini n.k.