Qualcomm waiburuza Transsion mahakamani, Transsion Holdings ni kampuni inayomiliki chapa maarufu za simu za Tecno, Infinix na Itel. Kampuni ya Qualcomm, mtengenezaji maarufu wa chips za simu, imedai kampuni ya Transsion imevunja haki miliki zake za kiteknolojia katika utengenezaji wa simu zao.
Qualcomm wamesema kampuni ya Transsion inatengeneza baadhi ya simu zake zikija na teknolojia bunifu za Qualcomm bila leseni stahiki. Ingawa simu nyingi za Tecno na Infinix zinatumia chips za MediaTek badala ya Qualcomm, inaonekana kuna teknolojia nyingine inayomilikiwa na Qualcomm ambayo hutumika kwenye simu hizo.
Hili lina maana gani?
Kwa upande wa Qualcomm, shtaka hili lina lengo la kulinda uvumbuzi wao na teknolojia walizozitengeneza. Kampuni nyingi hutumia leseni ili kutumia teknolojia ya Qualcomm kihalali, na inaonekana Qualcomm wanaona Transsion wameshindwa kufanya hivyo.
Kwa upande wa Transsion, shtaka hili linaweza kuathiri biashara zao kwa njia mbili. Kwanza, endapo mahakama itaipata Transsion na hatia, inaweza kulazimika kulipa Qualcomm faini kubwa. Pili, uwezekano wa Transsion kuzuiwa kutumia teknolojia hiyo unaweza kuathiri uwezo wao wa kutengeneza simu mpya.
Changamoto za namna hii ni kawaida katika biashara za bidhaa za elektroniki kama simu, kompyuta na zingine nyingi. Mara nyingi wahusika huweza kumaliza tofauti zao nje ya mahakama kwa makubadiliano ya muda mrefu ya kibiashara.
Wakati huo huo kampuni ya Phillips pia imefungua mashtaka ya aina hiyohiyo dhidi ya Transsion. Kutokana na ukuaji mkubwa katika soko la simu hasa za Tecno na Infinix, ikienda sambamba na nia yao ya kuingia katika masoko ya baadhi ya nchi Ulaya na Amerika ya Kusini – tutegemee kuona makampuni makubwa mengi zaidi kufuatilia zaidi utumiaji wa teknolojia zao katika simu za Transsion, kwa sasa inaonesha mafanikio yao yanakuja na wajibu wa kuhakikisha mikataba yao ya utumiaji wa baadhi ya teknolojia zenye hakimiliki (IPs) ipo safi.
Je, Hii Itaathiri Soko la Simu za Bei Nafuu?
Transsion imekuwa ikifahamika kwa kutengeneza simu janja za bei nafuu katika nchi nyingi zinazoendelea, zikiwemo Tanzania. Shtaka hili linaweza kuathiri uwezo wa Transsion kuendelea kutoa simu bora kwa bei nafuu. Ukiukaji wa sheria na faini zinazowezekana kutokea zinaweza kuongeza gharama ya uzalishaji wa simu zao.
Kuna uwezekano wa mambo mawili kutokea;
- Transsion inaweza kufanya makubaliano na Qualcomm na kupata leseni ya kutumia teknolojia inayolalamikiwa.
- Vinginevyo, Transsion inaweza kulazimika kutafuta njia mbadala ya kutumia teknolojia hiyo bila kuvunja sheria.
Hatima ya Transsion
Uamuzi wa mahakama utakuwa muhimu katika kuona hatima ya Transsion. Endapo watashinda kesi hii, wanaweza kuendelea na biashara zao kama kawaida. Hata hivyo, ikiwa watashindwa, wanaweza kukabiliwa na adhabu kubwa na changamoto ya kuendelea kutengeneza simu bora kwa bei nafuu.
No Comment! Be the first one.