Je unakumbuka tulichoandika katika mambo yanayokuja na Windows 10?Tulitaja mwisho wa kivinjari (browser) cha Internet Explorer (IE) kinachomilikiwa na kampuni ya Microsoft na ambacho kimekuwa kinakuja kikiwa kishawekwa kwenye kompyuta/laptop zote zinazotumia programu endeshaji za Windows.
Kampuni ya Microsoft imeeleza wazi kwa sasa ya kwamba kivinjari hicho kitabadilishwa na kivinjari kipya ambacho kinatambulika kwa jina la Spartan.
Kwa muda mrefu programu ya IE ilikuwa ikimilika asilimia kubwa zaidi ya utumiaji lakini kuja kwa Firefox na baadae kivinjari kutoka Google cha Chrome vilileta ushindani mkubwa kiasi cha kufanya IE kuonekana kama programu ya kizamani zaidi ambayo haijaendana na wakati.
IE ilishika umaarufu na kuchukua sifa ya kuwa programu moja muhimu katika masuala ya intaneti tokea miaka ya 1990. Ubora wake enzi hizo uliifanya kuwa ndiyo moja programu muhimu zaidi katika kuwawezesha watu kutumia intaneti.
Kufahamu kwa undani kuhusu toleo la Windows 10 na kivinjari kipya cha Spartan bofya -> Windows 10 Itapatikana ‘bure’ Kwa Mwaka Mmoja!
Je Spartan itafanikiwa kupunguza kasi za vivinjari vya Firefox na Chrome katika utumiaji? Kwa mtazamo wetu hili linategemea kwani upendeleo mkubwa ambayo Spartan itapata ni kuweka tayari kwenye kompyuta nyingi za toleo lijalo la Windows. Kama itakuwa bora na nzuri zaidi basi wengi wanaweza kujikuta wakiendelea kuitumia bila kushusha vivinjari vingine, lakini je Spartan itakuwa bora zaidi? Muda utatuambia.
No Comment! Be the first one.