Mwaka mmoja umepita tangia kumalizika rasmi kwa mauzo ya biashara za simu za Nokia kwa kampuni kubwa ya Microsoft, na sasa habari zinatoka ya kwamba Nokia wamejipangakurudi tena katika soko la simu janja.
Mara ya mwisho sababu kubwa za Nokia kushindwa kuhimili ushindani mkubwa kutoka Apple na simu za Android ilikuwa ni kutokana na kosa la kutobadilika haraka pale soko na teknolojia ilipobadilika, wakapoteza nafasi yao katika soko.
Hata hivyo usitegemee kuona simu hizo zinazokuja kutoka Nokia kufanana na zile ambazo watumiaji wengi wa simu tulizizoea katika miaka ya 90 hadi ile ya 2000. Ujio huu utakua wa aina yake kwani kampuni hiyo inadai iko tayari kuleta mabadiliko makubwa katika simu janja. Nokia iko tayari kutoa leseni ya jina na ubunifu kwa kampuni ambayo iko tayari kuendesha shughuli za uzalishaji, mauzo na usambazaji kwa ujumla. Hali hii ni tofauti na jinsi walivyokuwa wanafanya zamani ambapo walikuwa wanabuni , kutengeneza na kuingiza sokoni simu zao wenyewe.
Kitengo cha utengenezaji simu, au biashara ya simu ya Nokia ilinunuliwa na Microsoft kwa takribani dola bilioni 7 za Kimarekani, yaani zaidi ya Sh Trilioni 13.6 za Kitanzania.
Unachotakiwa kufahamu kuhusu Nokia;
- Nokia imekuwepo kwa miaka mingi na biashara zingine zaidi ya utengenezaji wa simu tuu
- Waliuza biashara yao ya utengenezaji simu tuu kwa Microsoft na hivyo kampuni ya Nokia bado ipo ila imeendelea kujikita katika biashara zingine kubwa katika teknolojia za mawasiliano
- Inasemekana katika mkataba wake wa kimauzo na Microsoft wameipa Microsoft haki ya kutumia jina la Nokia kwenye simu kwa muda flani tuu na tayari tumeshaona Microsoft wameanza kuacha kulitumia na sasa wanatoa simu wanazoziita Lumia zaidi bila neno ‘Nokia’.
- Katika manunuzi hiyo kwa sasa Microsoft inahaki miliki nzima ya majina maarufu ya simu zilizokuwa zinatengenezwa na Nokia kama vile ‘The Lumia’, ‘Asha’ na simu zilizokuwa zinatumia jina la X.
Inasemekana katika mkataba wake wa mauzo ya biashara ya simu kwa Microsoft, Nokia watakuwa huru kutoa simu kuanzia mwisho wa mwaka huu wakitumia jina la Nokia tena.
Wiki iliyopita Nokia wamenunua kampuni nguli ya teknolojia ya mawasiliano ya nchini Ufaransa ifahamikayo kama Alcatel-Lucent linalojihusisha na mawasiliano ya simu kwa dola bilioni 16.6 za kimarekani. Mikataba inasemekana kukamilika mwaka 2016, ununuzi huu ulikuwa muhimu zaidi kwa ajili ya kuweza kuipa Nokia ufanisi zaidi na uwezo wa kushindana na kampuni nyingine maarufu iliyojikita katika teknolojia ya mawasiliano, Ericsson.
One Comment