Mwaka jana tuliandika kuhusu roboti Flippy. Flippy ni roboti maarufu aliyetengenezwa kwa ajili ya kufanya kazi katika migahawa, inayotengeneza msosi maarufu mijini – unaokwenda kwa jina la Burger/baga.
Flippy aliwekwa kazini katika mgahawa maarufu wa Cali Burger tawi la jijini Pasadena huko California na kuchukua nafasi ya mpishi binadamu katika kutengeneza burger.
Ila baada ya kufanya kazi kwa muda wa siku moja ilibidi roboti Flippy kuzimwa kwa muda, ili kufanyiwa maboresha na kuhakikisha roboti huyo aweze kutengeneza burger nyingi zaidi kuliko sasa hivi. Kumuongeneza kasi yake ya utengenezaji burger.
Kwa sasa katika mgahawa huo bado roboti huyo yupo eneo lake la kazi lakini amezimwa na kibao cha tangazo kinachosema ‘nitaendelea kupika hivi karibuni’ – ‘cooking soon’ kikiwa kimewekwa.
Inasemekana habari kuhusu roboti huyo zilifanya wateja wengi zaidi kwenda katika mgahawa huo na hivyo kuathiri utendaji wa roboti huyo. Akajikuta anapata wateja wengi zaidi kuliko uwezo wake.
Roboti Flippy ametengenezwa na kampuni inayokwenda kwa jina la Miso Robotics. Lengo kuu la roboti Flippy ni kusaidia kuongeza ufanisi na kupunguza gharama kwa wenye migahawa kwani kwa sasa watakuwa wamepunguza gharama za kufundisha wafanyakazi mara kwa mara kuhusu utengenezaji burger – inasemakana eneo la migahawa kama hii mara nyingi wafanyakazi huwa hawakai muda mrefu sana na hivyo kuna gharama nyingi katika kuajiri watu wapya na kuwapa mafunzo kwanza.
Roboti Flippy achukui nafasi zote za ajira, bado kuna kuwa na watu wanaohakikisha vitu vyote vinavyoitajika katika utengenezaji wa burger vipo katika hali nzuri na vinawekwa katika eneo ambalo roboti huyo huvichukua na kisha kufanya upishi wa burger.
Kwa sasa roboti Flippy alikuwa na uwezo wa kutengeneza hadi burger 2000 kwa siku. Miso Robotics wanalenga la kuongeza zaidi.