Tumezoea vitu vingi sana kutengenezwa katika umbo la miraba minne au mstatili na si katika simu tuu. Hii ni kwenye tableti, milango 🙂 , madirisha, TV, na vitu vingine vingi tuu. Ila hakuna aliyewahi kufikiri umbo la duara au mviringo jinsi gani litakuwa kwenye kifaa kama simu janja.
Kuna simu ya kwanza kabisa yenye umbo la duara kutengenezwa itaingia sokoni hivi karibuni. Simu hiyo inaitwa Runcible, na inatengenezwa na kampuni ndogo huko Marekani.
Kwa nini wameamua kutengeneza simu ya umbo la mviringo?
Kwa kifupi mwanzilishi wa kampuni ya Monohm inayotengeneza simu hizi Bwana Heorge Arriola anadai lengo kuu ni kuleta utofauti katika kizazi ambacho simu zimekuwa zikiwafanya watu wengi zaidi kutofurahia maisha ya kila siku nje ya simu zao. Yaani milio ya taarifa fupi (notifications) kutoka mitandao ya kijamii kwenye simu na tableti zao zinawafanya watu watumie muda mwingi zaidi wakitazama simu zao kuliko kufanya mazungumzo na watu waliokaribu nao.
Kiubunifu wamechagua umbo hili kutoka kwenye saa ambazo kwa muda mrefu zilikuwa na umbo la duara zaidi na pia kutoka kwenye umbo la dira yaani ‘compass’ ambazo kwa miaka mingi mamia kwa mamia zimekuwa zikitengenezwa katika umbo la mduara.
Je nini cha kitofauti?
Kwanza kabisa simu hii itakuwa inatumia programu endeshaji (OS) ya Firefox OS, hii ni OS mpya inayotengenezwa na kampuni ya Firefox.
Pili, ili kukuepusha wewe kupoteza muda sana katika mitandao ya kijamii kila baada ya kutumia taarifa fupi yaani ‘notifications’ wao wataondoa hili na kufanya ‘icon’ yaani ile sehemu ya kubofya kufungua app husika kuongezeka ukubwa kila unapotakiwa kupata taarifa fupi. Kwa hiyo njia pekee ya wewe kutaka kujua kama kuna ‘notifications’ mpya itabidi utazame kioo cha Runcible, hii itasaidia kwani kumbuka hakutakuwa mlio wala mtetemeko (vibration) pale unapokuwa na ujumbe mpya katika mitandao ya kijamii.
Tatu, itadumu miaka na miaka! Kivipi? – Wametengeneza katika hali ambayo vifaa mbalimbali vya ndani kama vile kamera, RAM, na vingine vingi kuweza kubadilishwa ili kuongeza uwezo wake na hivyo kuondoa ulazima wa wewe kununua mpya kisa ina uwezo mkubwa zaidi wa RAM, kamera na mengineyo. Wenyewe wanadai wanataka simu hii iweze kupita kwenye familia kizazi kwa kizazi 🙂
Nne, je ujapenda muonekano flani wa vazi lake (cover)? Nalo utaweza badilisha kiurahisi tuu.
Umbo lake sio kubwa sana na unaweza kuiweka kwa urahisi mfukoni, kwenye shati au suruali n.k. Pia utaweza kuunganisha na kamba ya mvuto au cheni kama ukitaka.
Sifa zingine?
Teknolojia nyingine maarufu kama vile WiFi, LTE, Bluetooth na NFC zitapatikana kama kawaida.
Je itapatikana lini?
Bado hawajasema itapatikana lini ila wanadai ni miezi chache tuu ijayo na usitegemee ianze kuuzwa duniani kote. Wataanza na nchi chache na kukua taratibu.
Angalia picha zaidi hapa;
[metaslider id=2819]
Picha na ‘The Verge‘ na vyanzo vingine!
No Comment! Be the first one.