Rwanda wazindua simu janja za kisasa na bei nafuu zilizotengenezwa nchini humo. Uzinduzi huo uliofanyika jumatatu, ulifanywa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Kampuni ya Mara Group imetambulisha simu zake mbili, Mara X na Mara Z.
Simu ya Mara X itauzwa kwa Franc 175,750 za Rwanda (takribani $190, au Tsh 436,000/=) wakati Mara Z itauzwa kwa Franc 120,250 za Rwanda (takribani $130, au Tsh 300,000/=).

Simu hizo zinatarajiwa kuleta ushindani kwa simu zilizo sokoni kwa mujibu wa maelezo ya Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Mara, Ashish Thakkar ambaye amesema watazalisha simu milioni 2 kila mwaka.
Kiwanda cha Mara Group kinauwezo wa kutengeneza hadi simu 1,200 kwa siku. Kina jipa sifa ya kuwa kiwanda cha kwanza barani Afrika ambacho kinatengeneza kweli bidhaa ya simu ndani ya nchi ya Afrika – yaani kiwanda cha ‘manufacturing’, viwanda vingine vya simu nchini Misri, Naijeria, Ethipia na Afrika Kusini vinasifa ya kuwa viwanda vya ‘assembly’. Yaani ni viwanda ambavyo vinahusisha zaidi uungaji wa vipuri/parts zinazotengenezwa nje ya Afrika – hasa hasa China n.k.
Kiwanda cha Mara Group nchini Rwanda kinatengeneza vipuri mbalimbali hapo hapo bila uhitaji wa kuagiza nje. Suala hili linahakikisha unafuu wa bei za simu zao.
Ili kuhakikisha wananchi wanaweza kununua simu hizo kampuni hiyo tayari inafanya mazungumzo na mabenki ili watu waweze kuchukua simu na kulipa taratibu kwa muda wa miaka 2. Mfumo ambao ni maarufu katika nchi zilizoendelea.
Kampuni ya Mara Phones, ipo chini ya kampuni kubwa ya Mara Group inayomilikiwa na Ashish Thakkar. Ashish Thakkar alizaliwa Uingereza na kuhamia Rwanda akiwa mtoto mdogo. Alianzisha kampuni ya Mara Group kipindi ana umri wa miaka 15, kwa sasa ana miaka 38.
