Watu wengi hufikiria kuwa data tunayotumia ipo angani—katika “wingu” (cloud). Ukweli ni kwamba, haipo angani bali chini ya bahari. Intaneti tunayofurahia kila siku husafiri kwa kasi kupitia nyaya nyembamba sana zilizowekwa chini ya bahari, zikielekeza data kutoka bara moja hadi jingine kwa sekunde chache tu.
Njia Isiyoonekana Inayounganisha Dunia
Hivi sasa, zaidi ya kilomita 1.2 milioni za nyaya za chini ya bahari ndizo zinazobeba mawasiliano yetu ya mtandaoni. Nyaya hizi ni kama mishipa ya damu ya intaneti, zikipeleka data kutoka New York hadi Sydney, kutoka London hadi Hong Kong. Bila hizi nyaya, mawasiliano ya mtandaoni yangekuwa ya polepole au hata kutowezekana kabisa.
Zamani, makampuni yalikuwa yakishirikiana kuweka nyaya hizi, kama barabara kuu inayotumiwa na magari tofauti. Lakini hivi sasa, kampuni kubwa kama Google, Amazon, Meta (Facebook), na Microsoft zinajenga nyaya zao binafsi. Mfano halisi ni mradi wa Google uliounganisha Marekani na Chile—ambapo Google ina kituo kikubwa cha kuhifadhi data barani Amerika Kusini.
Je, Nyaya Hizi Huundwaje na Kuwekwa Baharini?
Safari ya nyaya hizi huanzia viwandani, ambako hutengenezwa kwa umakini mkubwa. Kila waya huwekewa vikinga maalum ili kuhimili shinikizo na mazingira magumu ya baharini. Baada ya kutengenezwa, hupelekwa bandarini na kupakiwa kwenye meli maalum kama Durable, yenye urefu wa futi 456, ambayo hubeba nyaya hizo na kuzitandaza taratibu baharini.
Wakati mwingine, nyaya hizi hulazimika kupita kwenye kina kirefu cha bahari, zikikabiliana na changamoto kama matetemeko ya ardhi, meli zinazopita juu yake, au hata papa wanaotafuna nyaya! Ndiyo maana zinafanyiwa majaribio makali kabla ya kusafirishwa.
Kwa Nini Nyaya za Chini ya Bahari ni Muhimu?
Ingawa teknolojia ya setilaiti ipo, bado haijafikia kasi na ufanisi wa nyaya za chini ya bahari. Setilaiti zinaweza kusaidia, lakini kwa video za moja kwa moja (live streaming), simu za video, na huduma za wingu (cloud), nyaya hizi ni uti wa mgongo wa intaneti ya dunia.
Kwa hiyo, kila unapobofya linki, kutazama video, au kutuma ujumbe kwa rafiki yako nje ya nchi, kumbuka: data haipo angani—ipo chini ya bahari, ikisafiri kupitia nyaya zisizoonekana lakini zinazoshikilia dunia yetu ya kidigitali pamoja.
Timu ya uandishi wa Kona ya Teknolojia ingefurahi kupata sapoti yako ili iendelee kukuletea habari na maujanja mbalimbali.
Wezesha bando kwa kutuma kiasi chochote kupitia Selcom, kwenye simu yako bofya *150*50*1# kwenye namba ya malipo weka 60751369 jina litakuja TEKNOKONA.
No Comment! Be the first one.