Bwana Elon Musk, mkurugenzi na msimamiaji mkuu wa teknolojia katika kampuni inayojihusisha na teknolojia za Anga ya Space X, amesema kwamba wanalengo la kuhakikisha safari ya kwanza ya kwenda kwenye sayari ya Mirihi (Mars) kufikia mwaka 2024 iwe imeshafanyika.
Safari hiyo yenye lengo la kuhusisha teknolojia yao ya kisasa ya ndege na roketi zinazoweza kutumiwa bila kuharibika itakuwa ya kiaina yake. Kwa muda mrefu sasa Bwana Elon Musk kupitia kampuni yake ya anga ya Space X wamekuwa wakiweka rekodi nzuri za kiteknolojia katika huduma za anga.

Mafanikio ya Space X:
- Mwaka 2015, walifanikiwa kuwezesha roketi kutua tena duniani, ikiwa imesimama baada ya kupeleka mzigo katika anga za juu – satelaiti. Kawaida kabla ya maendeleo haya kwenye sekta ya anga roketi zilikuwa zikitumwa angani, zinarudi zikiungua na kuharibika na kuwa vipande vipande na kukosa sifa ya kuweza kutumika tena.
- Mei 27 mwaka huu walifanikiwa kwa mara ya kwanza kupeleka wanasayansi wa anga katika kituo cha anga cha kimataifa (International Space Station). Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa shirika lisilo la kiserikali kufanikisha hili. Kutokana na gharama za teknolojia ya zamani kuwa kubwa kwa muda mrefu Marekani ilikuwa inapeleka wanasayansi wake kupitia shirika la anga la Urusi, hivyo hili lilikuwa jambo kubwa kisiasa nchini Marekani.
Soma Habari nyingi zaidi za Space X -> Teknokona/Space X
Kwa sasa Space X wanaendelea na matengenezo na majaribio ya ndege yao inayotambulika kwa sasa kwa jina la SpaceShip, ni ndege hii ndiyo inategemewa kuwezesha safari hiyo ya kwenda kwenye sayari ya Mirihi.
Elon Musk, amesema safari ya kwanza haitahusisha binadamu. Ila ni lengo lao kuhakikisha ukuaji wa ubunifu na teknolojia katika kampuni ya Space X unakuwa wa haraka zaidi ili kuwezesha safari za binadamu ndani ya miaka michache baada ya safari hiyo ya kwanza.
No Comment! Be the first one.