Dunia inaingia kwenye hatua ambayo Akili Mnemba haitakuwa tu mashindano ya kampuni kama OpenAI, Google na wengine. Nchi pia zinataka kuwa na nafasi katika kuamua teknolojia hii itajengwa na kutumika kwa misingi gani.
Katika mazingira hayo, Sam Altman, CEO wa OpenAI, ameitaka Marekani kuongoza juhudi za kimataifa za kuweka viwango vya kiufundi kwa mifumo ya juu ya Akili Mnemba.
Altman Anataka Dunia Iwe Na Viwango Vinavyofanana
Kwa OpenAI, tatizo linaweza kutokea ikiwa kila nchi itatengeneza viwango vyake. Mfumo wa Akili Mnemba uliotengenezwa Marekani unaweza kuwa na namna tofauti ya kupima usalama, kutoa taarifa za matukio hatari au kutathmini uwezo wake kuliko mfumo uliotengenezwa China au Ulaya. Ndiyo maana OpenAI inapendekeza viwango vinavyoweza kutumiwa na nchi mbalimbali, pamoja na njia zinazofanana za kupima mifumo hiyo na kuripoti matukio hatari.
Marekani Na China Ziko Kwenye Mashindano
Hapa ndipo suala linakuwa kubwa zaidi. Marekani inaona Akili Mnemba kama teknolojia muhimu kwa uchumi na usalama wa taifa, wakati China nayo inaendelea kuongeza uwezo wake katika eneo hilo. Tofauti zao zinaonekana pia kwenye suala la udhibiti wa teknolojia na upatikanaji wa chips za hali ya juu.
Kwa upande mwingine, mazungumzo kati ya Washington na Beijing kuhusu usalama wa Akili Mnemba tayari yanaendelea, yakiwemo mapendekezo ya kuwa na njia ya mawasiliano wakati kunapotokea tukio kubwa la usalama.
Trump Anataka Marekani Ibaki Mbele
Rais Donald Trump amekuwa akipinga wito wa kupunguza kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba kwa hofu kwamba kufanya hivyo kunaweza kuipa China nafasi ya kusogea mbele. Hivyo, msimamo wa Trump unaweka mkazo kwenye kuendeleza teknolojia huku Marekani ikijaribu kulinda nafasi yake katika mashindano hayo.
Hii inatengeneza mjadala tofauti na ule wa Altman: si tu jinsi ya kuendeleza AI, bali pia jinsi ya kuweka usalama bila kupunguza kasi ya ubunifu.
Trump anatarajiwa kukutana na Rais wa China Xi Jinping mjini Washington wiki hii, huku Akili Mnemba ikiwa miongoni mwa masuala muhimu yanayozunguka mazungumzo yao. Mkutano huo unakuja wakati nchi hizo mbili tayari zimeanza kujadiliana kuhusu usalama wa Akili Mnemba. Marekani imependekeza mfumo wa mawasiliano wa kushirikiana taarifa kuhusu matukio hatari yanayohusisha teknolojia hiyo.
Mjadala wa Akili Mnemba sasa umevuka mipaka ya kampuni za teknolojia. Unahusu pia viwango, usalama na nani atakuwa na ushawishi katika hatua inayofuata ya teknolojia hii. Altman anataka Marekani iongoze mchakato huo. Trump anataka Marekani ibaki mbele kwenye mashindano. Na China nayo haitaki kubaki nyuma. Sasa dunia inasubiri kuona kama ushindani huu utaishia kwenye mashindano ya teknolojia pekee, au utafungua pia njia mpya za ushirikiano.
Timu ya uandishi wa Kona ya Teknolojia ingefurahi kupata sapoti yako ili iendelee kukuletea habari na maujanja mbalimbali.
Wezesha bando kwa kutuma kiasi chochote kupitia Selcom, kwenye simu yako bofya *150*50*1# kwenye namba ya malipo weka 60751369 jina litakuja TEKNOKONA.
No Comment! Be the first one.