Sarafu ya kidigitali ya Libra kutoka Facebook na washirika wake wanaojenga umoja na kampuni inayojitegemea wanayoiita Libra Association imeendelea kupita kwenye changamoto.
Hivi karibuni Paypal, ambao walikuwa ni wadau wengine kwenye umoja huo walijitoa, na sasa imefahamika makampuni makubwa katika teknolojia za mihamala ya pesa yaani MasterCard na Visa pia wajitoa kwenye umoja huo pia.
Sarafu ya Libra ina malengo gani?
Kama zilivyo sarafu zingine za kidigitali kama vile Bitcoin, sarafu ya Libra ina lengo la kurahisisha manunuzi na utumaji fedha kwa njia ya mtandao kwa watumiaji mbalimbali duniani kote.
Facebook wamejikuta wakipingwa vikali na mashirika ya usimamiaji fedha hasa hasa kwa Marekani, Uingereza, Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi. Wasiwasi mkubwa ikiwa ni kama Facebook na washirika wao wataweza kulinda data za watumiaji wa huduma hiyo – kumbuka tayari Facebook inaskendo nyingi za utumiaji usio sahihi wa watumiaji wa huduma zao – na pia uvujaji wa data za watumiaji wa huduma zao.

MasterCard na Visa wote wamesema wataendelea kuangalia kwa ukaribu maendeleo na mpango wa Libra. Kama vyombo vya usimamizi wa fedha vya mataifa mbalimbali wakiupokea mpango huo basi na wao huko mbeleni wanaweza kurudi tena kwenye kushirikiana na Facebook.
Alhamisi ya tarehe 17/10/2019 kundi la mataifa saba ya juu kiuchumi – G7, pia walitoa mawazo yao dhidi ya mpango wa Libra. Katika taarifa yao iliyoripotiwa na vyombo kama Reuters na vinginevyo mawaziri wa fedha wa nchi hizo wamesema mpango wa kuleta sarafu za kidigitali kama Libra usimamishwe kwanza na kuruhusiwa pale tuu ambapo vyombo vya fedha kama kimataifa kama IMF na Benki ya Dunia vitakapojiridhisha juu ya usalama wake.
Ingawa mpango wa Libra tayari unaendelea kama kawaida kuna uwezekano mkubwa ukasimamishwa kilazima na mataifa yenye nguvu kiuchumi kama Marekani na Umoja wa Ulaya. Suala la fedha limekuwa nyeti kwa mataifa haya na kutokana na ukubwa wa mtandao wa kijamii wa Facebook – zaidi ya watumiaji bilioni 2, wana wasiwasi kuwa sarafu hii ikifanikiwa basi ni sarafu/fedha zao ndio zitakazo poteza nafasi yake katika biashara.
Je una mtazamo gani juu ya fedha za kidigitali? Soma mengi kuhusu Facebook na Libra hapa;