Sasatel ilivyoingia katika biashara mwaka 2009 watu wengi walifurahi na walitegemea mapinduzi makubwa katika huduma ya mawasiliano hasa hasa katika eneo la data (intaneti) ila kitu kimoja tuu ndio kilionekana kutia shaka, nacho ni utumiaji wa mfumo wa CDMA. CDMA ni teknolojia inayotumiwa na TTCL pia, ipo tofauti na GSM inayotumiwa na mitandao mingine ya simu.
Hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa taarifa ya kuwa kuna uwezekano wakaifutia leseni kampuni ya Dovetel (T) – wamiliki wa Sasatel, kutokana na kutotumia leseni zake ipasavyo, na hii ni pamoja na uongozi wa kampuni hiyo kutotokea kujitetea tarehe 23 Mei mwaka huu walipotakiwa kufanya hivyo.
Sasatel inayoendeshwa chini ya kampuni mama iitwayo Dovetel ilipoanza wengi walitegemea mengi kwani muasisi na mwenyeketi wake ni Mtanzania atambulikaye kwa jina la Prof Peter Chitamu, yeye alianzisha kampuni mama ya Dovetel mwaka 2005.
Je ni wapi walipokosea?
Sehemu moja kubwa kwa mtazamo wangu ni uchaguzi wa kuingia kwa mfumo wa CDMA badala ya wa GSM, au kuingia na mifumo yote kwa wakati mmoja – kitu anachofanya Zantel. Kuja na mfumo wa CDMA unamaanisha inabidi kuhangaika kuwauzia watu zaidi ya huduma tuu, bali kuwaambia wanunue simu nyingine tena. Na hapo ni jambo gumu sana, na hii ni kutokana na kujua ya kwamba usipopendezwa na huduma inamaanisha hutaweza kuitumia simu husika.
Ubovu wa timu ya utangazaji biashara (marketing) na kutosambaa kwa haraka kwa huduma. Kwa kiasi kikubwa tunaona kampuni ya Smile inafanikiwa katika biashara yake, na hii inatokana na juhudi kubwa katika kujitangaza. Ushindani ni mkubwa lakini kama wewe ni mpya ni lazima ujipange kufanya jihada kubwa kutambulika kama ndiye bingwa mpya katika huduma husika, na hapa Sasatel walijitahidi lakini hawakujitutumia sana.
Kosa la tatu ni kutosambaza huduma kwenye miji mingine inayokuwa kwa haraka kama ilivyotegemewa. Kwa Dar es Salaam tuu baadhi ya maeneo yenye watu wengi kama kimara mwisho na mbezi kimara huduma ilikuwa bado ya utata, huduma ilichelewa kusambaa na hii inaweza ikawa ni kutokana na kutojipanga vizuri kibiashara u kifedha.
Matatizo ya Kifedha – Pia linaweza likawa limechangia, inaonekana walioweka pesa zao katika kampuni ya Dovetel hawakuweka za kutosha na walitegemea kupata mafanikio ya haraka na hivyo kuiweka kampuni hiyo katika wakati mgumu. Katika uchunguzi wetu inaonesha adi kufikia mwishoni mwa mwaka 2011 kampuni ya Sasatel ilikuwa ishapata hasara ya zaidi ya Tsh Bilioni 50 (Dola Milioni 30 za US)*, na kuanzia kati kati ya mwaka 2012 tayari kampuni ya Dovetel ilishaanza kuachia baadhi ya mali kama majengo kulipa pesa za wawekezaji wa huko uingereza. Na pia walishaanza harakati za kuuza kampuni hiyo moja kwa moja.*
Kwa sasa kampuni mpya za mawasiliano ya simu kama Smart na Smile Tanzania zinabidi kujifunza kutokana na makosa ya Sasatel.
*ft.com| The Citizen, Tanzania
No Comment! Be the first one.