Teknolojia ya uhifadhi ni ya ajabu kidogo siku hizi, zamani mtu ukiwa na GB 8 tuu kuzijaza ilikuwa ni shughuli. Cha kushangaza siku hizi mtu anaweza kuacha kununua kifaa kwa sababu tuu kina uhifadhi mdogo, ukiuliza unaweza ukashangaa ujazo huo mdogo (kwake) ni GB 16.
Kwenye soko la simu hili jambo lipo sana. Ili kuendana na soko hilo watengenezaji wa aina mbalimbali za simu janja wanajitahidi kuhakikisha wateja wao wanapata simu bora tena zile zenye uhifadhi mkubwa.
Kumbuka siku hizi kuna App zinakula hadi GB 1 katika simu janja zetu. App nyingi za michezo (magemu) hasa yale yenye uwezo mkubwa wa ‘graphics’ yanakuwa yna ujazo mkubwa na kadri unavyozidi kulicheza linazidi kuongezeka ukubwa wake. Ndio! ukubwa wake unaongezeka kwa kuwa linakuwa linafadhi taarifa zako mbali mbali kama vile ‘level’ uliyopo, vikombe ulivyochukua n.k.
Kulingana na kuwa mambo yako mengi sana siku hizi katika simu janja zetu basi uhifadhi haiwezi kutosha kamwe. Ukiachana na App bado hujajaza miziki na video unazozipenda kuanzia miaka ya 70 au 80. Pia kumbuka muziki au video nzuri inachua uhifadhi mkubwa kuliko ile ambayo sio nzuri.
Kampuni ya Samsung hivi karibuni imetangaza kuwa inatengeneza memori kadi (SD Cards) za kutumika kwenye simu zenye ukubwa wa GB 256. Mpaka sasa memori kadi (SD Cards) zenye ukubwa zaidi zimeonekana kuwa ni 128 ambazo ndio zipo katika soko kuu.
Ukiachana na ukubwa wa uhifadhi (BD 256), vimemori hivi ni vidogo sana na ni vidogo ukilinganisha na zile za kawaida. Jambo hili linakuwa ni msaada tosha kwa watengenezaji wa simu kwani (kama ni kidogo sana) wanaweza wakakiweka popote wanapoona panafaa.
Lakini ni Samsung tuu hata makampuni makubwa kama Apple yanajikita vikali kuhakikisha simu zake za iPhone zinapata ujazo wa uhifadhi mkubwa. Usije ukashangaa hata simu mpya za iPhone zikawa zina ujazo wa uhifadhi wa GB 256.
Jambo ambalo liko wazi ni kwamba hakuna sababu ya kampuni lolote kubwa la kutengeneza simu kuwapatia wateja wake simu zenye ujazo wa uhifadhi wa GB 16. Jambo liko wazi kuwa uhifadhi huo ni mdogo sana, labda tuu kwa watu amabo hawapendi kuwa na mambo mengi katika simu zao lakini hata hivyo hao watu wakinogewa na baadhi ya vitu bado hizo zitakuwa hazitoshi tuu.