Mtandao wa kijamii wa Snapchat umezidi kuipa Facebook wakati mgumu kibiashara, hii ni baada ya kuzidi kupata watumiaji wengi wanaoangalia video kwa siku. Snapchat imekuwa ikipata mashabiki wengi kwa haraka sana na watumiaji hao kutumia kwa sana huduma zao, hali hii inahatarisha utawala wa Facebook katika soko.
Ukuaji huu wa Snapchat unatishia utawala wa Facebook katika uwanja wa mitandao ya kijamii kwa sababu Facebook na mitandao mingine ambayo hatuilipii inategemea mapato yake kutoka katika matangazo. Hii ina maana kwamba mtandao ambao unawafikia watu wengi zaidi na watu hao kuwa ni watumiaji wa mara kwa mara zaidi – utaweza kuuza nafasi za matangazo kwa bei kubwa zaidi, na hivyo utaweza kukusanya mapato makubwa zaidi na hivyo kuweza kukua zaidi.
Snapchat wametangaza kufikia idadi ya mitazamo (video views) bilioni 6 ya video kila siku, hii ni mara tatu zaidi ya idadi ya kila siku katika mwezi wa tano. Hii ni bilioni mbili nyuma ya video zinazotazamwa katika mtandao wa siku nyingi wa Facebook ambao wiki iliyopita ulitangaza kufikia mitazamo ya video bilioni 8 kila siku.
Kwa kiswahili chepesi ni kwamba video za Snapchat zinapata watazamaji wengi kwa siku na kama hali itaendelea kama hivi basi watawazidi hata Facebook, hii itasababisha Snapchat iweze kupata ofa nzuri zaidi kimatangazo na hivyo kupata mapato makubwa zaidi kutokana na kiwango kikubwa cha watu kutumia mtandao huo wa kijamii – ‘high engagement’. Hivyo ni wazi kwamba Facebook ipo katika wakati mgumu kuhakikisha kwamba watumiaji wake hawamezwi na Snapchat hasa katika masuala ya utumaji na uangaliaji wa video fupi.
Vipi Umekwishajiunga na Snapchat? kama ndiyo, je unauonaje mtandao huu mpya? na kama jibu ni hapana kwanini?
One Comment