Soko la simu janja linaonekana kutokua kwa mara ya kwanza katika miaka mingi. Makampuni matano ya juu kwa uiingizaji wa simu janja sokoni kati ya Januari hadi Mwezi Machi 2016 ni Samsung, Apple, Huawei, OPPO na Vivo.
Kwa haraka haraka utagundua Oppo na Vivo ni wageni kabisa katika orodha hii, na kwa wengi ni makampuni yasiyo na jina huku Afrika Mashiriki. Kampuni za simu za Oppo na Vivo zimewaondoa Lenovo na Xiaomi katika orodha ya waingizaji simu wakubwa 5 katika soko la simu janja duniani.
Data zilizotolewa na shirika la kimataifa la utafiti (IDC – International Data Corporation) zinaonesha kutokuwepo kwa ukuaji wa mahitaji ya simu janja kwenye soko katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu (Januari – Machi).
0.20% – Asilimia ya ukuaji wa idadi nzima ya simu janja zilizoingia sokoni katika kipindi cha Januari/Machi 2016 ukilinganisha na kipindi cha Septemba/Disemba 2015.
Kutokuwepo na uhitaji wa simu janja kwa wingi kwenye soko kumesababishwa na uwepo wa simu kibao katika soko ambazo bado hazinunuliki…na inasemekana wateja wengi wa simu janja katika nchi zilizoendelea tayari wanamiliki simu za uwezo wa juu sana na hivyo kuwafanya wasibadilishe simu mara kwa mara ukilinganisha na zamani.
Suala hili limewaathiri zaidi Apple katika ujio wa simu zao za iPhone 6S, watumiaji wengi wa toleo lililopita, iPhone 6, hawakuona umuhimu wa kununua iPhone 6S na matokeo yake kwa mara ya kwanza Apple wamejikuta wakiuza simu chache zaidi katika kipindi hichi.
Nafasi ya nne na tano imechukuliwa kwa mara ya kwanza na makampuni ya Oppo na Vivo huku wakiyapita Lenovo na Xiaomi. Vivo Mobile na Oppo Electronics ni makampuni ya nchini China na simu zake zinapatikana kwenye mataifa machache nje ya Uchina.
Inaonekana makampuni ya utengenezaji simu ya nchini Uchina yanapata changamoto kubwa katika kukuza biashara hiyo kimataifa…na inaaminika wakifanikiwa katika hilo basi wana nafasi kubwa ya kukua zaidi. Kwa sasa Huawei ndio mfano mkubwa wa mafanikio hayo. Na wengi wanaona uwezo wao wa kuweza kutoa simu za ubora wa juu wa kufananishwa na ata Samsung ndio umewasaidia kuendelea kushikilia nafasi ya tatu.
Je una mtazamo gani wa hali ya uwepo na bei ya simu janja zinazopatikana kwa sasa madukani?
Chanzo: Indian Express na Mitandao mbalimbali