Kama wewe ni kama mimi, yani unatumia mtandao mara kwa mara kwenye harakati zako za kila siku na katika kupata taarifa na habari, basi utakukubaliana nami kwamba kuna kipindi unaweza kujikuta umepotea kabisa kwenye mtandao. Pengine hata inafika muda ukajiuliza – hivi nilikuwa nataka kufanya nini na hii simu (au laptopu) kabla ya kuingia mtandaoni?!
Maisha yetu yanabadilika, na kadri siku zinavyoenda, uwezo wetu wa kuwa makini na kitu kimoja kwa wakati mmoja unaweza kuathiriwa na ndio maana huduma za ‘Soma Baadae’ zimeanza kupata umaarufu duniani na hata zinatumika na majina maarufu kama Facebook na Mozilla katika siku za karibuni.
Huduma ya ‘Soma Baadae’ (yani ‘Read it Later’ au ‘Save it for Later’ kwa lugha ya malkia) ni huduma inayompa mtumiaji wa mtandao uwezo wa kuhifadhi pembeni kitu alichokiona mtandaoni wakati anafanya kitu kingine cha muhimu zaidi wakati huo ili aweze kurudi baadae na kukisoma alichokihifadhi.
Mapema mwezi huu wa sita, Mozilla walitangaza sasisho kwenye kivinjari chao cha Firefox liliongeza huduma ya ‘Pocket’ moja-kwa-moja kwenye kivinjari hicho kwa watu wote. Pocket ni huduma ya ku-soma baadae iliojizolea umaarufu duniani kote kwa kurahisisha maisha na kuwaokolea muda watu mbalimbali wanaotumia mtandao. Hivi sasa ukipakia Mozilla Firefox kwenye kompyuta yako, inakuja moja kwa moja na Pocket.
Huduma ya Pocket inashusha chochote unachotaka kusoma baadae ili uweze kusoma bila intaneti. Huduma hii inaweza kutumika kwenye simu na tabiti pia na ina uwezo wa kuoanisha (‘synchronise’) makala zako kati ya kompyuta, tabiti na simu yako ili uweze kuzipata popote unapoenda. Huduma ya Pocket na nyingine za aina yake, kama ‘Instatpaper’ zainapendwa pia kwa kuwa zinaongeza umakini wa kusoma habari na makala. Zinafanya hivi kwa kuondoa mambo mengi yaliyo kwenye kurasa za kawaida za mtandao na kuonesha mwili wa habari, makala, video au sauti inayohitajika na mtumiaji. Kama wewe ni kama mimi na unatumia mtandao kupata taarifa nyingi, utapenda kutumia huduma hizi. Anza kutumia huduma ya ‘Soma Baadae’ sasa.
Facebook wao wana aina tofauti ya huduma ya ‘Soma Baadae’ kupitia kipengele cha ‘Save it for later’ ambacho utakipata kwenye ‘taarifa’ kutoka kurasa uzipendazo kama Teknokona.
Unapohifadhi taarifa hizi, unaweza kurudi baadae na kuzikuta chini ya chaguzo la ‘Save’ ambalo lipo upande wa kushoto kwenye kurasa yako ya Mwanzo ya Facebook. Utakuta uliyoyahifadhi yamepangwa katika makundi ya linki, picha, video, vitabu, shoo na kadhalika. Ingawa hata kwa kutumia hii unaweza kupotea kwenye facebook au mtandao tena, itakusaidia usiweze kukosa kuhifadhi kitu chochote ukionapo facebook kwa ajili ya baadae.
Anza kutumia huduma za ‘soma baadae’ sasa na utaona umuhimu wake. Ufanisi wako utaongongezeka, elimu na ujuzi wako utaongezeka na hatimaye utaona zinakuokoa katika dunia ambayo imejaa na taarifa nyingi zinazokuja kwa wingi kila sekunde!
Pocket | Instapaper | Evernote Clearly | Facebook Save
No Comment! Be the first one.