Huduma ya intaneti ya Starlink ndani ya Kenya 😎 . Huduma ya intaneti ya kasi kwa njia ya satelaiti kutoka kampuni ya SpaceX imeanza kupatikana rasmi nchini Kenya.
Muanzilishi wa SpaceX na Starlink, mmoja wa matajiri wakubwa duniani, Bwana Elon Musk alifurahia taarifa rasmi ya upatikanaji wa huduma hiyo kupitia akaunti yake ya Twitter akisambaza ujumbe kutoka akaunti rasmi ya Starlink. Huduma ya intaneti ya Starlink inaendeshwa kwa kutumia maelfu ya satelaiti zinazozunguka dunia huku zikipokea na kutuma moja kwa moja huduma ya intaneti kwa watumiaji wanaohitaji kifaa cha kielektroniki spesheli cha ungo, kama vile vya TV za satelaiti – cha SpaceX kikiwa ni kidogo zaidi kwa umbo.
Kwa sasa kwa wastani huduma ya intaneti ya satelaiti ya Starlink inapatikana kwa kasi ya Mbps 25 – 100 kwa kushusha (downloads) na Mbps 5 – 10 kwa kupandisha (uploads). Kwa wastani kasi ya kupakua (download) ni Mbps 97.23, ambayo inaweza muwezesha mtumiaji kushusha filamu ya ubora wa HD ndani ya dakika moja.
Starlink kupatikana Tanzania lini?
Miezi kadhaa nyuma Bwana Elon Musk alisema ujio wa huduma hiyo nchini Tanzania umekwama kutokana na changamoto ya kupata kibali, alisema wanasubiri kibali ili waweze kuruhusu huduma yao kuanza kupatakana nchini Tanzania. Akizungumza na ITV Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Elon Musk hakuwa na mpango wa kuweka ofisi ya Starlink nchini katika hatua yake ya kuwekeza katika utoaji wa huduma ya intaneti kupitia satelaiti.
Je Starlink wanahitaji ofisi?
Kwa kiasi flani mfumo wa biashara wa makampuni kama haya huwa ni kuwa na wasambazaji rasmi katika nchi husika, mfano ata Kenya tayari makampuni rasmi (ya Kenya) yameshaanza kujitambulisha kama wasambazaji rasmi wa huduma hiyo. Wasambazaji hawa pia ndio wanakuwa chanzo cha kwanza cha huduma kwa wateja, nje ya hapo Starlink pia ina mfumo wa huduma kwa wateja kwa njia ya mtandao.
Tunasogeaje kutoka hapa?
Tayari kwa nchi majirani huduma ya intaneti ya Starlink ishaanza kupatikana na wadau kunufaika nayo nchini Rwanda na Msumbiji. Nje ya watumiaji wa kawaida, mfumo wa huduma ya intaneti kwa kwa njia ya satelaiti una manufaa makubwa sana kwa biashara zilizo kwenye sekta ya kilimo, utalii na uchimbaji madini – kwa kuwa kuna wafanyabiashara wa sekta hizi ambao huwa wanajikuta wanaendesha shughuli zao katika maeneo ambayo yako mbali na huduma za uhakika za intaneti kupitia mitandao ya simu.
Intaneti kwa njia ya satelaiti
Huduma ya intaneti kwa njia ya satelaiti inawafikia watu wa maeneo mengi zaidi kwa kuwa satelaiti – hasa kwa maelfu yake, zinafikia na kuweza kurusha mawasiliano katika maeneo makubwa kuliko vifaa vya mawasiliano vinavyoweza kufungwa ardhini kwenye minara.
Tunaweza kuchelewa lakini hatuwezi kushindana na teknolojia, tunategemea muda si mrefu tutaweza kuwakaribisha rasmi Starlink Tanzania. Kwa sasa kampuni inayotoa huduma ya intaneti ya kasi kwa mfumo wa satelaiti inayopatikana maeneo yote nchini Tanzania na ikiwa na ofisi rasmi nchini ni Konnect. Tutegemee ujio wa Starlink kuongeza ushindani na kuwapa wateja nafasi zaidi ya kuchagua huduma zilizo bora na zinazokidhi mahitaji ya wateja wa aina zote.
No Comment! Be the first one.