Unaikumbuka simu ya Tecno Boom J7? Simu ambayo naamini itakuwa inashikilia rekodi ya kimauzo kwa Tecno kwa mwaka jana bila ubishi. Tecno Boom J8 ni muendelezo wa familia ya simu za Boom kutoka Tecno.
Fahamu uwezo wake, muonekano wake n.k katika uchambuzi huu.
![Tecno Boom J8](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/05/tecno-boom-j9-teknokona.jpg)
Shuka chini kuangalia uchambuzi wa Tecno Boom J8 wa kutumia Video!
Tecno Boom J7 ilipokelewa vizuri sana kutokana na ubunifu na upatikaji wake katika bei iliyokuwa ya nafuu ukilinganisha na simu zenye sifa kama yake kutoka makampuni mengine.
Nimefanikiwa kuitumia simu ya Boom J8 kwa siku kadhaa na yafutayo ni niliyoyaona;
Ni nini cha kipekee zaidi katika Tecno Boom J8?
![Muonekano - Tecno Boom J8](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/05/Muonekano-simu-ya-tecno-boom-j8-1024x607.jpg)
Kwanza – TeknoKona tunaweza chambua matoleo makuu matatu ya simu za Tecno kama ifuatavyo; kuna zile zinazolenga soko la bei ya juu – Tecno Phantom, kuna zile kwa ajili ya watumiaji wa aina zote, Tecno Camon, na hizi za Tecno Boom – ambazo zinalenga watu wa kisasa zaidi, wapenzi wa muziki na mambo ya kisasa.
Sifa/Uwezo wa Boom J8 kwa ufupi
- Programu endeshaji: Android 5.1 spesheli ya HiOS
- Teknolojia za mawasiliano: 2G/3G/4GLTE (GSM/WCDMA/LTE) ( LTE:Band B3/7/20)
- Prosesa: Quad-core
- Kioo (Display): Inchi 5.5 HD IPS Touchscreen
- Kamera: Megapixel 13 nyuma, MP 5 mbele (selfi), zote zinapiga Flash
- Diski ujazo (storage): GB 16GB pamoja na RAM ya GB 2
- Uwezo wa betri: mAh 3000
- Teknolojia zingine – Wi-Fi, BT, GPS
- Unaweza tumia memori kadi (Micro SD) ya hadi GB 128
Android 5.1 – HiOS
Simu hii inakuja na toleo la programu endeshaji la Android 5.1 lakini lilofanyiwa maboresho ya muoneakano uliopewa jina la HiOS. Muonekano huu wa HiOS ukijumlisha na RAM ya GB 2 iliyokwenye simu hii inaifanya simu hii kuwa na kasi nzuri katika utendaji wake.
![hiOS](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/05/HiOS-tecno-576x1024.png)
Na kama katika matoleo yake ya simu zake za sasa, Tecno wameweka mfumo wa kuendelea kupata masasisho (updates) kwa simu hii. Baada ya kuunganisha na intaneti nilipata taarifa (notification) ya kwamba natakiwa kuupdate.
Muonekano
Ukiishika kwa mara ya kwanza lazima utakubali ya kwamba simu hii ni maboresho makubwa kutoka Tecno Boom J7. Boom J8 ni nyembamba na inastahili sifa ya kuwa kati ya simu janja nyembamba zaidi za ukubwa wa inchi 5.5.
Kutengeneza kasha lake (housing) imetumika plastiki pamoja na aluminiamu ambayo inasaidia kuipa simu muonekano wa kuvutia.
Kamera
Kwenye Tecno Boom J8 kuna maboresho kadhaa kutoka toleo la J7. J8 inakuja na kamera ya nyuma ya MP 13 na ya selfi MP 5, ukilinganisha na J7 ambayo ilikuwa na kamera ya nyuma ya MP 8 na ya selfi ikiwa ni MP 2.
![simu ya tecno boom j8](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/05/IMG_20160514_083832-1024x576.jpg)
Kamera zimekuja na teknolojia ya maboresho ya ubora wa picha – optical image stabilization. Pia kamera ya nyuma inauwezo wa kupiga picha za panorama. App ya kamera inauwezo wa kutambua (‘detect’) sura na pia inakupa nafasi ya kuboresha vitu kama mwanga n.k kabla ya upigaji picha.
Ukaaji wa Chaji (Betri)
Katika majaribio niliyofanya nilifanikiwa kuangalia muvi mbili kupitia app ya VLC niliyoipakua pamoja na kusikiliza muziki kwa zaidi ya masaa mawili na bado nikawa na kiwango cha chaji cha zaidi ya asilimia 40%.
Tecno Boom J7 ilikuja na betri ya mAh 2020 wakati Boom J8 imeongezwa maradufu kiwango cha betri na kufikia mAh 3000. Kwa kipimo hichi utaweza kufanya mambo mengi ndani ya siku bila ya kuwa na wasiwasi na suala la chaji. Pia kupitia uwezo wa ‘Ultra lower power mode’ utaweza kufanya simu yako kutumia kiwango kiduchu zaidi cha chaji kwa apps muhimu tuu pale unapojua utakuwa mbali na uwezo wa kuchaji kwa muda mrefu.
Muziki na Boom Player
![Tecno Boom J8 Boom Player](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/05/Boom-player-tecno.jpg)
App ya Boom Player ni moja ya kitu kilichoboreshwa zaidi katika simu ya Tecno Boom J8. Kwa muda mrefu app ya Boom Player ilikuwa kama app nyingine yeyote ya kawaida ya kusikilizia muziki, lakini kwa sasa app ya Boom Player imepewa uwezo mkubwa zaidi.
Sifa/uwezo wa App ya Boom Player
- Kusikiliza muziki uliyohifadhi kwenye simu yako (au kupitia memori kadi yako – na video pia)
- Kusikiliza nyimbo mbalimbali za kimataifa na za Tanzania kupitia njia ya ku’stream
- Pia tazama video ulizohifadhi kwenye simu yako
- Tazama pia video za nyimbo mbalimbali za kimataifa na za Tanzania kupitia njia ya ku’stream
- Utaweza pia kushiriki katika mazungumzo juu ya wimbo au video flani na watumiaji mbalimbali wa app hiyo kutoka nchi zingine wanaotumia app hiyo
- Utaweza kulike na kushare nyimbo unazopenda n.k kwenda kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook
- Kudownload nyimbo kabisa kabisa itabidi ulipie
Ingawa ukinunua simu hii inatakiwa pia kupewa headphone za bure ila bado kupitia app ya Boom Maxx utaweza kuchagua mipangilio ya sauti kulingana na aina ya earphones/headphones unazotumia.
App ya Boom Player imeunganishwa vizuri na simu kiasi ya kwamba ukiwa unasikiliza muziki basi kuna eneo la chini tu baada ya display litakuwa linawaka waka kutokana na jinsi mdundo wa muziki unavyopiga.
[Soma Pia -> Kuhusu shindano linalohusisha Boom Player ambalo mshindi atapelekwa nchini Ufaransa katika jiji la Paris}
Na majaribio tuliyofanya ya kusikiliza mzuki kupitia Boom Player na pia app zingine kama vile Shuttle na DeaDBeef ambazo ni moja ya apps nzuri kabisa za bure bado tuligundua kuna ubora flani nyimbo zinasikika vizuri zaidi kwenye Boom Player.
Tecno Boom J8 pia imetengenezwa kwa teknolojia za juu za mfumo wa sauti – hivyo iwe kupitia spika za simu yenyewe au pale unapotumia headphones kiwango kizima cha sauti kinachotoka ni cha kiwango cha juu. Boom Player kama app spesheli ya simu hii ipo katika uwezo mkubwa wa kutumia teknolojia hizi kuhakikisha kiwango cha uchezaji muziki ni cha juu.
Tazama Video zetu za Uchambuzi;
Bei:
Wakati Boom J8 imekuja na maboresho mengi bado bei yake haijaenda mbali sana na ile iliyokuja na Boom J7, simu ya Boom J8 inapatikana kwa kati ya Tsh 380,000/= hadi Tsh 450,000/=, hivyo kama ni bajeti basi ukiwa na Tsh 400,000 unaweza ukawa poa. (Kwa Kenya Ksh 14,999/- Ksh 16,999/=)
Uchambuzi umekuwa mrefu kutokana na upatikanaji wa simu hii na hivyo kupata muda mrefu wa kuitumia vizuri.
Je umeshatumia simu ya Boom J7? au J8? Tuambie mtazamo wako juu ya maboresho yaliyokuja katika Boom J8. Na usisite kutuambia simu gani nyingine ungependa kuifahamu kwa undani.
Kwa habari zaidi zinazohusu simu -> teknokona.com/teknolojia/simu/