Tokea kampuni ya Microsoft inunue teknolojia na huduma nzima ya Skype kumekuwa na mabadiliko na maboresho mbalimbali yaliyofanyika lakini uamuzi huu mpya unaonekana ndio utasaidia sana katika kuifanya Skype iendelee kuwepo kwa miaka mingi zaidi na ata kuweza kushindana na huduma zingine mpya kama vile Google Hangout kutoka Google. Kuanzia sasa watumiaji wa Skype nchini Marekani na Uingereza wameshaanza kuweza kutumia Skype kupitia vivinjari (browser) vyao, na uwezo huo utasambaa taratibu kwa watumiaji wote duniani.
Kwa sasa uwezo wa kuchati na kupiga simu umekuwa unapatikana kupitia programu/app zao kwa ajili ya kompyuta, tableti na simu na tunaona uamuzi huu wa kuruhusu utumiaji wa Skype bila kupakua programu yao kwenye kifaa chako utazidi kurahisisha na kuongeza utumiaji wa huduma hiyo.
Hivi karibuni tuu Skype walileta uwezo mpya unaovutia sana, watumiaji wanaozungumza lugha tofauti wataweza kuchati au kuongea na maongezi yao kuweza kutafsiriwa muda huo huo. Soma -> Skype – Wakuwezesha Kuchati na Kuzungumza na Watu Mbalimbali KTK Lugha Zao Bila Wewe Kuzifahamu!
Tegemea kuweza kutumia Skype yako hivi karibuni tuu kupitia kivinjari chako. Huduma hii ya kwenye kivinjari wameiita jina la ‘Skype for Web’, na katika utumiaji wake kwa sasa itakubidi kupakua kiprogramu kidogo (plugin) kwenye kivinjari chako ila tayari wamesema wanafanya kazi kuondoa kabisa ulazima wa kufanya hivyo. Kwa sasa utaweza kutumia huduma hiyo kwenye vivinjari vya Internet Explorer, Chrome, Safari or Firefox.
Je wewe ni mtumiaji wa Skype? Umefurahishwa kiasi gani na uamuzi huu?
No Comment! Be the first one.