Unapoendesha gari katika barabara ambayo haina taa changamoto ni nyingi, kuna watembea kwa miguu pembeni ya barabara, kuna wanyama kama mbwa paka na wengineo ambao wanaweza wakakusababishia ajali ambayo hukuitegemea. Changamoto hizi huenda zikawa zimeondolewa kabisa, na moja ya njia kuu imeonekana ni kwa kutumia taa janja kwenye magari.
Kampuni ya Ford (ambao ni watengenezaji wa magari) inatengeneza mfumo wa taa ambao utakuwa zaidi ya taa za kawaida, mfumo huu unategemewa kumsaidia dereva kupata taarifa zaidi ya vitu vilivyo mbele na pembezoni mwa barabara. Mfumo huu wa taa janja utahusisha camera za infrared na teknolojia ya kutambua alama za barabarani ambavyo kwa pamoja vitasaidia kupata taarifa za muhimu.
Taarifa hizi muhimu zinazopatikana pamoja kwa msaada wa GPS zitaweza kutengeneza picha za video ambazo zitamuonesha mtu au mnyama aliye karibu na gari, kamera za infrared huweza kutambua viumbe kama binadamu na wanyama kwa kutumia mionzi ambayo binadamu na wanyama huitoa.
Pamoja na kumsaidia dereva kwa kumpa taarifa juu ya waenda kwa miguu na mengineyo huu mfumo utaweza pia kukumbuka kona miinuko na mabonde ya barabara ambayo gari hiyo imekwisha pita hivyo kumpa nafasi dereva kuweza kuwa muangalifu zaidi. Kwa lugha nyepesi ni kwamba mfumo huu utalifanya gari lako kukusaidia kujua kuwa hapo unapokaribia kuna kona ama muinuko iwapo tu ulikwishalipitisha njia hiyo.
Audi nao pia hawako nyuma katika mbio hizi kwani pamoja na kuendelea kuiboresha mifumo yao ya taa sasa wanafikiria kuja na mfumo wa taa ambao utakuwa unayafuatisha macho yako kule yanakoangalia, yaani ukiangalia kushoto basi na taa zinaelekea huko zaidi. Upo hapo? 🙂
Tuandikie kama una maoni, mawazo au hata maswali… Endelea kutembelea TeknoKona!
No Comment! Be the first one.