Voice over LTE kwa kifupi VoLTE ni teknolojia inayotumia intaneti (yaani data) kufanikisha huduma zingine kama vile upigaji na upokeaji wa simu. Leo pata kufahamu zaidi kuhusu VoLTE kwa undani.
Vifupi vya kuelewa
- LTE – Long Term Evolution
- VoLTE – Voice of LTE
Historia
Teknolojia za 2G, 3G, na ata 4G inayotangazwa na mitandao mingi ni teknolojia zinazotegemea mifumo miwili ya mawasiliano ya (1) sauti kwa ajili ya kutoa huduma za kupiga na kupokea simu – pia pamoja (2) mfumo wa kusafirishia data (yaani huduma ya intaneti)
Teknolojia ya 4G inakuja katika mifumo miwili, mmoja ni wa WiMAX na mwingine kisasa zaidi ni wa LTE – Mifumo hii imetengenezwa kwa ajili ya usafirishaji wa data (huduma ya intaneti) na maboresho ili kuuwezesha mfumo wa LTE kuweza kupiga na kupokea simu ndio umeleta VoLTE.
Sasa VoLTE ni nini?
Ila VoLTE (Voice over LTE) ni kinyume chake, hii teknolojia inayotegemea mfumo wa mawasiliano ya data (intaneti) kuruhusu huduma zingine zote. Hii ikimaanisha ata kupiga na kupokea simu zinakuwa kama app yeyote kwenye simu yako kwa sasa – sauti itasafirishwa kupitia data/intaneti.
VoLTE ni teknolojia mboresho iliyotengenezwa baada ya kuona mapungufu flani katika teknolojia ya usafarishaji data (intaneti) ya LTE.
Kuna Umuhimu wowote wa VoLTE?
VoLTE imekuwa muhimu kwani siku hizi matumizi namba moja ya mawasiliano ni data na hivyo ikaonekana ni muhimu badala ya kuongeza gharama kwa watoa huduma kwani ilikuwa inawabidi wawe na mifumo miwili – kwa ajili ya mawasiliano ya sauti (upigaji simu) na pia kwa ajili ya huduma za intaneti – Data ya kasi zaidi (LTE)
Ujio wa VoLTE ina maana sasa kutapunguza gharama za kuwekeza katika huduma zote mbili – mawasiliano ya simu na pia intaneti. Na kizuri zaidi ni kwamba VoLTE inaongeza ubora pia wa sauti katika huduma za kupiga simu.
Kama mtumiaji wa kawaida hili linamaanisha nini?
Kwa sasa ni mtandao wa Smile tuu ndio waliokuja na teknolojia hii kwa sasa na mitandao mingine yenye huduma ya 4G bado inategemea mifumo ya zamani ya mawasiliano ya upigaji simu huku wakiongezea mifumo mingine spesheli kwa ajili ya data.
Kuna faida katika suala la gharama kushuka kwa watoa huduma ila kwa haraka haraka ni vigumu kufahamu kama gharama zitashushwa sana na watoa huduma. Kwani kwa sasa hautachajiwa katika mfumo wa maongezi kwa sekunde/dakika bali utachajiwa kwa /KB au /MB unazotumia.
Kama vile ambapo kwa sasa huduma nyingi za intaneti unazigharamia kwa MB basi ata upigaji na upokeaji simu katika mfumo wa VoLTE utalipiwa hivyo hivyo.
Kama umechunguza kwa sasa ata katika mitandao ya 3G na ata inayojiita ni ya ‘4G’ ukiwa unapiga simu huduma za intaneti huwa zinapotea kwa muda wote wa maongezi – hii ni kwa sababu mifumo hiyo inaruhusu kitu kimoja kwa wakati mmoja – data(intaneti) au upigaji simu tu, kimoja kwa wakati.
Katika VoLTE upigaji simu utaendelea bila kuathiri ufanyaji kazi wa app zingine zinazotumia data/intaneti pia – kwani ata upigaji simu utakuwa unatumia mfumo huo huo wa intaneti.
Mitandao inayokuja na teknolojia ya VoLTE inaleta ushindani mkali kwa huduma zingine kama vile FaceTime, Skype, WhatsApp na zingine zinazotumia huduma ya intaneti katika upigaji na upokeaji simu. Kwa mitandao ya simu ni rahisi wao kuporesha huduma zao na ata kutoa vijiofa kwani wao ndio wamiliki wa miundo mbinu ya huduma ya intaneti kwa wateja wao.
Unaweza kusoma zaidi kuhusu tofauti za teknolojia za mawasiliano ya 2G/EDGE, 3G, 4G na LTE hapa -> Fahamu tofauti kuu kati ya teknolojia za 2G, 3G, 4G, n.k
Je una maoni gani juu ya teknolojia hii? Tuambie na tuulize kupitia eneo la comment