NFC ni nini? Kama umeshawahi kuangalia hardware specifications za simu janja zinazoongoza kwenye soko katika kipindi chochote miaka kadhaa iliyopita basi kuna nafasi nzuri ushawahi kuona neno ‘NFC’ likiwa limeorodheshwa kwenye orodha hizo.
Lakini licha ya kuwa teknolojia hii imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa lakini bado haijawa swala la kawaida kwenye simu janja, zote ni baadhi tu ya simu janja zinazokuja na teknolojia hii.
NFC ni nini hasa? Kuiweka kiurahisi ni njia inayotumika kuhamisha data kutoka kifaa kimoja kwenda kingine vilivyo na ukaribu kwa kuwasiliana bila kutumia wire (wireless) wala uhitaji wa mtandao wa intaneti. Ni rahisi, haraka na inafanya kazi kimaajabu.
Inafanya vipi kazi?
NFC imetokea kwenye teknolojia ya radio frequency identification (RFID), chip ya NFC inafanya kazi kama sehemu ya kiungo cha wireless link. Inapoamlishwa (activated) na chip kutoka kifaa kingine, sehemu ndogo ya data kati ya vifaa hivyo viwili huanza kusafirishwa zinapowekwa umbali mfupi kati yao.
Hamna haja ya kutumia ‘pairing code’ kama ilivyozoeleka kwenye teknolojia ya Bluetooth kuunganisha vifaa viwili ili kusafirisha data kati yao, NFC inatumia chip zilizopo ndani ya vifaa husika.
Inatofauti gani na teknolojia ya Bluetooth?
Unaweza ukafikiria kwamba “Mbona Bluetooth inaweza kufanya hivyo pia?” Uko sahihi. Lakini hata ukiilinganisha na Bluetooth LE, NFC inatumia nguvu (power) ndogo zaidi. Hii ni muhimu ukizingatia tunategemea miaka kadhaa mbeleni simu janja kuchukua nafasi ya pochi (wallets) zetu, na maisha ya betri kwenye simu janja zetu yatakua muhimu zaidi.
Bila kusahau, kuunganisha vifaa viwili kwa kutumia Bluetooth inaweza kuwa jambo linalosumbua kichwa kidogo, Kwanza kukifaanya kifaa kionekane na kifaa kingine….kutafuta kifaa kingine kama kipo umbali sahihi na kisha ndo kuanza kusafirisha data kati ya vifaa hivyo viwili.
Unawezaje kutumia teknolojia hii kwa sasa?
Chip za NFC zilizopo ndani ya kadi karadha (credit card) kwa ajili ya malipo mbali mbali sio swala jipya. Lakini kwa kipindi cha hivi karibuni jambo linalovutia zaidi katika matumizi ya NFC ni uwezo wake kuifanya simu janja yako iweze kutumika kama pochi ya kidigitali.
Karibu watengenezaji wote wa mfumo endeshi(operating system) wana programu zao zinazotoa huduma tofauti za NFC. Watumiaji wa mfumo wa Android wana wigo mkubwa wa kuchagua programu hizi za NFC, kwa mfano Google Wallet na Samsung Pay ambazo programu zote zinafanya kazi sawa.
Ingawa programu ambayo watumiaji wengi wa mfumo wa Android wanapenda kutumia na kuifurahia inaitwa Android Beam, ambayo ilianza kutumika katika toleo la Ice Cream Sandwich 4.0 kama programu inayowezesha kuhamishiana picha, namba za simu na maelekezo (directions) kwa kushika simu mbili kwa pamoja katika umbali mdogo.
Simu za iPhone 6 na iPhone 6 Plus ndo zilikua simu janja za kwanza kutoka Apple kuwahi kuwa na mfumo wa NFC, lakini kwa simu za Apple zinakubali programu moja tu ya Apple Pay, ambayo inawawezesha watumiaji wake kufanya malipo ya bidhaa na huduma.