Baada ya kuingia katika ulimwengu wa teknolojia na simu janja wengi tumekutana na majina haya ya teknolojia za mawasiliano za 1G, 2G, 3G, 4G na 5G. Haya ni majina ambayo yana maana kubwa katika uwezo wa mtandao wako aidha katika huduma za intaneti au ata zile za ujumbe mfupi na upigaji simu.
Tuanze na hiyo G: G ina maana ya “Generation” au kwa lugha yetu ni “Kizazi”. Vizazi hivi vimegawanyika katika makundi 5 [ 1G, 2G, 3G, 4G na 5G ] ili kujua upo kwenye kundi lipi la kizazi kwenye simu janja, unapowasha data/mtandao kupata internet huonekana juu kwenye alama za minara (bars).
Namba ya kizazi/Generation inapoongezeka ndivyo spidi na uwezo wa mtandao wako pia unaongezeka. Tutaangalia kila kizazi/Generation maana yake, namna inavyofanya kazi na uwezo wake.
1G (1st Generation)
Teknolojia hii ilitambulisha mawasiliano ya kwanza ya simu yasiyo tumia waya (wireless cellular network). Hii bado ilitumia teknolojia ya analojia ambayo ilidumu toka 1979 mpaka miaka ya mwanzo ya 80’s baada ya 2G kutambulishwa.
1G ilikuwa na spidi ya 2.4Kbps. Spidi ambayo leo hii ukipewa ni bora usiwe na internet kabisa, Teknolojia hii ilikuwa na mtandao hafifu sana na ubora wa mazungumzo ulikuwa chini sana. Mbaya zaidi haikuwa na usalama kwani mtu yeyote mwenye kifaa kiitwacho Radio scanner anaweza kusikiliza mazungumzo yenu.
Kufeli kwa kizazi cha kwanza cha Mawasiliano (1G) katika gharama zake na ubora kulipelekea uvumbuzi wa kiazi cha pili (2G).
2G (2nd Generation)
Kizazi hiki kilikuja chini ya viwango vya GSM (Global System for Mobile Communicatios). GSM ni teknolojia ya kidijitali ya simu ambayo iliongeza zaidi usalama na ubora wa mawasiliano, Kupitia hii teknolojia ya 2G kulitokea mabadiliko makubwa sana ya tamaduni za mawasiliano.
Kwa mara ya kwanza watu waliweza tuma jumbe fupi (SMS) na picha kupitia simu zao. Yote hii iliwezeshwa na 2G. Kipindi inaanza ilikuwa na spidi ya 9.6Kbps na ikasaidia kampuni za mawasiliano kuwekeza pesa zaidi kuboresha mawasiliano kwa kuongeza minara ya mawasiliano.
Baada ya maboresho hayo 2G iliweza kufika spidi mpaka 64Kbps na kuleta kitu unachoitwa EDGE (Enhanced Data Rates for GSM Evolution), yaani ile “E” ambayo huwa unaona kwenye mtandao wako. EDGE iliweza kusaidia 2G kufikia spidi ya 500Kbps.
Kizazi cha pili cha Mawasiliano (2G) kilisaidia na kuboresha huduma za mawasiliano watu waliweza kutuma picha, jumbe fupi (SMS) na hata matumizi ya jumbe za kimtandao kama Email.
3G (3rd Generation)
Hapa ndipo viwango vile vya mtandao wa leo vilitokea. 3G ilianza kutengenezwa miaka ya 2000’s na iliboresha spidi ya 2G zaidi ya mara 4. 3G iliitwa H (HSPA) ilimaanisha kwamba mtu anaweza kupata mtandao wa internet kutoka mahali popote pale duniani. Maana yake ni kwamba kabla ya hapo watu hawakuweza kuperuzi kurasa za mitandao (Websites) kutokea popote alipo bali mpaka awepo sehemu maalamu zilizowekwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Spidi ya 3G ilifika 144Kbps – 2Mbps. Spidi hii ilipelekea kuendesha vikao vya video kimtandao (Video Conferencing), Kuangalia video mtandaoni (Video Streaming) pamoja na VoIP (VoIP ni simu kupitia internet kama zile za whatsapp).
Kupitia kizazi cha tatu cha Mawasiliano (3G) tuliona mabadiliko na maboresho makubwa ya Mawasiliano kwa njia ya internet, hapa tuliweza kufanya mikutano kimtandao, kuangalia video mtandaoni n.k
4G (4th Generation)
4G ililetwa kipindi ambacho watu huita “Streaming Era”. Ni kipindi ambacho watu wengi wamekuwa wakifatilita vitu kama kuangalia sinema/movie, mechi za mpira bila kuzipakua au kusikiliza hotuba au Tamasha flani Mbashara (Live streaming)
4G ilianza 2006 lakini ilipata umaarufu 2009 ilipokuja 4G LTE. Sababu kubwa ni ile spidi iliyotolewa na 4G. Spidi yake ni kati ya 100Mbps – 1Gbps. Kipindi tunahama 2G kwenda 3G ilikuwa ni rahisi kama kubadili tu sim card/laini ya simu katika simu yako. Katika 4G simu zilihitaji kutengenezwa katika namna ambayo zinaweza tumia mtandao wa 4G kitu ambacho kilipelekea mpaka gharama za simu kupanda sana, Japo 4G ni kiwango kipya cha mtandao, bado kuna baadhi ya maeneo wanapata tabu kutumia tekinolojia hii sababu ya ugumu wa kuongeza nguvu ya 4G kuwafikia.
5G (5th Generation)
Kama 4G bado haijagusa maeneo mengi inakuaje sasa tunakimbilia 5G?
Kiuhalisia 5G ilianza tengenezwa muda mrefu sana miaka iliyopita. Mvumbuzi wa Internet of Things (IoT) Kevin Ashton anasema Simu sio simu, ila ni kifaa cha IoT. (Internet of Things) IoT ni muunganiko wa vifaa vinavyotumia mtandao. Ukiwa na Feni nyumbani iliyounganishwa na mtandao utaweza iwasha ukiwa sehemu yoyote duniani. Huo ni mfano wa IoT.
Sababu ya uhitaji huo wa mtandao wa 5G ni kwamba 3G na 4G zisingeweza kutoa huduma ya kuunganisha vifaa vingi kwa wakati mmoja vinavyotumia internet . 5G inaspidi ya kuanzia 100Mbps mpaka 20Gbps. Kwa spidi hii ya mtandao na matumizi yake, tunakoelekea 5G itakuwa ndiyo tegemeo letu kwenye maisha ya kila siku.
Maboresho ya Teknolojia yanafanyika kila leo, leo Internet ni moja ya nyenzo maalumu kabisa kwenye maisha yetu ya kila siku, na wapo wengine ambao kazi zao zote hutegemea internet, hivyo basi ni muhimu kujua tulipotoka, tulipo na tunapokwenda, miaka kadhaa ijayo tutashudia maboresho makubwa sana Kimtandao.
No Comment! Be the first one.