Kama ushawahi kutaka kuweka mipangilio (settings) za barua pepe katika app au mtandao unaoweza pokea barua pepe basi lazima utakuwa ushawahi kukutana na maneno haya, yaani POP na IMAP. Je ulichagua ipi na kwa sababu zipi?
Leo fahamu tofauti zake na uzuri wa kila moja ili uweze kuchagua vema mbeleni utakapoitaji kufanya mipangilio ya barua pepe tena. 😉
Kirefu cha IMAP ni ‘ Internet Message Access Protocol’ wakati POP ni Post Office Protocol. Kwa maelezo mafupi hizi ni teknolojia za utaratibu unaokuwezesha kupata barua pepe zako ambazo zinahifadhiwa katika ‘server’ flani. Kupitia teknolojia hizi utaweza kusoma barua pepe zako katika sehemu nyingine nje ya ‘server’ husika kama vile kwenye app au programu za kompyuta kama Outlook, Thunderbird n.k. Na kwa kifupi hili ndilo jambo kubwa ambalo teknolojia hizi mbili zinafanana.
Teknolojia ya POP ndiyo ya kwanza kabisa na ilitengenezwa mwaka 1984. Teknolojia ya POP inakuwezesha kushusha barua pepe zako kwa ujumla wake kutoka kwenye seva husika bila kuacha kopi nyingine yeyote kwenye seva.
Teknolojia ya IMAP ilianza kutumika mwaka 1986, hii inakuwezesha kuona barua pepe zako kwenye app au programu ya kompyuta bila kufuta barua pepe husika kwenye seva. Yaani app au programu husika ni kama kioo cha barua pepe zilizopo kwenye seva. Unaweza fananisha teknolojia ya IMAP na teknolojia ya ‘Cloud’.
Je zinafanyaje kazi kwa undani pale unapozitumia?
Jinsi POP Inavyofanya Kazi:
- Inakuunganisha kwenye seva (‘server’)
- Inashusha (download) barua pepe zako mpya
- Inazihifadhi kwenye app au programu husika ya barua pepe
- Inafuta barua pepe zote zilizopo kwenye seva*
- Kisha inakata mawasiliano kati ya seva na app/programu (hadi hapo kutapokuwa na barua pepe mpya)
*Hii ndivyo jinsi ilivyotengenezwa, kufuta barua za kwenye seva, lakini baadhi ya app/programu zinaweza kukupa chaguo la kuacha nakala kwenye seva.
Jinsi IMAPÂ Inavyofanya Kazi:
- Inakuunganisha kwenye seva (‘server’)
- Inakuletea nakala (copy) habari/barua pepe kwenye app/programu na kuacha nakala nyingine kama kawaida kwenye seva
- Pia inaangalia mabadiliko ya barua pepe ulizofanya kwenye app/programu yako. Kama umefuta, n.k barua pepe flani basi mabadiliko kama hayo yanatumwa na kufanyika katika nakala za kwenye seva pia
- Kisha inakata mawasiliano kati ya seva na app/programu (hadi hapo kutapokuwa na barua pepe mpya)
Kwa mtazamo wa haraka tuu utagundua ya kwamba utendaji wa IMAP sio wa kirahisi na ni mrefu ukilinganisha na wa POP.
Faida za Kutumia POP ni Zipi?
Kumbuka POP inamaana sana kwa watu wanaotumia sehemu moja tuu (programu au app) kutazama na kujibu barua pepe zao. Faida zake ni zifuatazo:
- Barua pepe yako huwa inashusha ikiwa imekamilika na kuhifadhiwa kwenye app/programu husika. Intaneti haitajiki tena ili kuweza kuzisoma.
- Intaneti inaitajika kwa ajili ya kutuma na kupokea barua pepe mpya tuu
- Inasaidia kuokoa ujazo katika seva. (Seva nyingi zinakuwa na ukubwa rasmi mfano GB 1 au MB 500, na ujazo huu ukijaa barua pepe mpya haziwezi kuingia)
- Baadhi ya app/programu zinakupa uhuru wa kuhifadhi barua pepe yako kwenye seva
- Uwezo wa kuhifadhi/kupokea barua pepe kutoka kwenye akaunti mbalimbali kutoka kwenye seva tofauti.
Faida za Kutumia IMAP ni Zipi?
Nakukumbusha tena ya kwamba teknolojia ya IMAP inakuwezesha kupata barua pepe zinazohifadhiwa katika seva/mtandao flani. Â Wazo kubwa katika teknolojia hii ni kuwezesha app/programu tofauti na mbalimbali, na watu tofauti tofauti kuweza kutumia akaunti moja ya barua pepe. Maana kuu ni kwamba ata kama umeweka akaunti yako ya barua pepe kwenye app ya simu, tableti, kompyuta yako ya nyumbani na ya kazini kwenye programu/app zote utaweza kupata barua pepe zako bila wasiwasi. Ila kama umetumia POP basi barua pepe hizi zitaenda sehemu moja tuu, ile iliyounganishwa na intaneti pale ujumbe wa barua pepe unapokuja, ukiangalia kwenye zingine baada hutaukuta ujumbe huo.
Faida zake ni kama ifuatavyo;
- Barua pepe zako zinakuwa zimehifadhiwa kwenye seva, hivyo utaweza zipata kwenye kifaa chochote kipya
- Intaneti inahitajika kuweza kutumia barua pepe
- Inashusha barua pepe haraka zaidi kwani haishushi yote, inashusha kichwa cha habari tuu. Ukibofya barua husika ndipo programu/app yako itawasiliana na seva kupata nakala nzima ya ujumbe huo.
- Huna wasiwasi wa kupotea kwa barua pepe zako kwani ata app au programu zikiharibika au kifaa chako mfano kompyuta ikiibiwa kwabi barua zako ziko kwenye seva
- Inakusaidia kutokujazia nafasi (storage) kwenye simu au programu yako. Kwani haishushi kitu bila wewe kukitaka.
- Una pewa chague la kuhifadhi nakala zote kwenye app/programu yako
Sasa umeelewa tofauti, je utumie mipangilio (settings) zipi kati ya POP na IMAP?
Mara nyingi hii inategemea mambo kadhaa, tazama na uamue;
Tumia POP;
- Kama unataka kutumia huduma yako ya barua pepe kutoka kwenye kifaa kimoja tuu.
- Kama unatumia barua pepe mara nyingi zaidi ata kama hauna huduma ya intaneti saa nyingine.
- Kama seva yako ina nafasi wa ujazo mdogo. Kumbuka seva zote zinakuwa na kiwango cha ujuzo, mfano MB 500, GB 1 n.k
Chagua IMAP;
- Kama unataka kuweza kutumia barua pepe yako kwenye vifaa tofauti tofauti
- Kama una intaneti ya uhakika isiyo na shida
- Unataka uwe na uwezo wa kuangalia vichwa vya habari kwa haraka zaidi ata kama utasoma barua pepe hizo baadae kwenye kifaa kingine
- Kama uhifadhi wa kifaa chako ni mdogo, hasa hasa kwenye simu au tableti
- Kama unawasiwasi wa kupoteza kifaa chako au huwa unabadilisha sana.
No Comment! Be the first one.