Ijue Toshiba T1100. Ni takribani miaka 31 sasa na laptop ya kwanza duniani kuweza kuuzika kwa watumiaji wowote (mass market) na leo fahamu sifa zake.
Kabla ya mwaka 1985 tayari matoleo kadhaa ya laptop chache na zilizouzwa kwa mashirika machache kama vile jeshi n.k tayari yalishatoka lakini ni ujio wa laptop ya Toshiba T1100 ndio ukastahili sifa kamili ya kuwa laptop ya kwanza kabisa kuanza kupatikana sokoni.

Laptop hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Toshiba ya nchini Japan ilijipatia umaarufu na inachukuliwa kama moja ya laptop zilizoleta mabadiliko sana katika teknolojia na uanzashwaji wa utengenezaji wa laptop kwa ajili ya watumiaji wa aina zote.
Sifa zake za ndani kwa kipindi hicho zilikuwa zinazotosha tuu kwa watumiaji mbalimbali ingawa kwa sasa simu janja yako tuu itakuwa inauwezo mara maelfu kuizidi laptop hii.
Ilikuja na;
- RAM ya KB 256
- Prosesa – 4.77 MHz Intel Processor
- Haikuwa na ‘HDD’ – Hard disk, ilikuwa inatumia Floppy Disk
- Programu endeshaji ya MS DOS
- Ilikuwa na uzito wa kg 4.1

Ndani ya mwaka wake wa kwanza kupatikana Toshiba waliuza laptop hizo 10,000, nyingi zikienda barani Ulaya…na zikajipatia sifa ya kipekee kama laptop ya kwanza kuweza kutumika na watu kwa matumizi mbalimbali madogo na makubwa ukilinganisha na kabla ya hapo.
Kwa kipindi hicho mtu kumiliki laptop hiyo ilikuwa ni bonge la maendeleo, unaweza fananisha na mtu kumiliki laptop za kisasa kabisa za siku hizi kama vile MacBook Air, Surface n.k